Samia ataka Watanzania kuvilinda viwanda

09Aug 2019
Na Waandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
Samia ataka Watanzania kuvilinda viwanda

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi na Watanzania kuvilinda viwanda vilivyopo na vinavyoanzishwa kwa kutambua kuwa ni mali yao, na sio mali ya wawekezaji peke yao.

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Alisema ni vyao kwa sababu  bidhaa zinazozalishwa zinategemea malighafi ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na zinazozalishwa na wananchi na kuchangia ukuaji wa mapato ya mtu mmoja mmoja, mkoa na taifa.

Makamu wa Rais alisema hayo wakati akizindua viwanda vya kuchakata mazao ya jamii ya mikunde cha Mahashree Agro Processing kilichopo Mikese wilayani Morogoro na cha kuchakata mpunga cha Muruz Wilmer East Africa Miller l.t.d kilichopo Kihonda Manispaa ya Morogoro.

Samia aliwahimiza wananchi wa Morogoro kuilinda miradi mikubwa inayopita maeneo yao ukiwamo mkubwa wa reli ya kisasa, na umeme wa Rufiji unaotegemea maji yatokanayo na mabonde na mito ya Morogoro, hasa kwa kulinda mazingira ili umeme upatikane wa kutosha kusaidia viwanda vilivyopo na vinavyoanzishwa.

Alipongeza  hatua ya wawekezaji wa sasa wa viwanda kutafuta kwanza masoko kabla ya kuanza uzalishaji, na kuwahimiza wananchi kuchangamkia fursa ya kuzalisha kwa wingi mazao kwa vile tayari wana maeneo ya kuuzia bidhaa zao sambamba na kuuza kwenye masoko ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Licha ya Morogoro kuwa miongoni mwa maghala ya taifa ya chakula, Makamu wa Rais akashangazwa kuona bado mkoa huo ni miongoni mwa inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu, hivyo akahimiza mazao ya kunde kutumike pia kwa mahitaji ya soko la ndani.

"Mwaka juzi Tanzania ilikuwa na shida kubwa ya soko la mbaazi, kama kiwanda kama hiki (cha kuchakata mazao ya kunde) kingekuwapo kingesaidia kuondoa tatizo hili, kuwapo kiwanda hiki hawatanunua tu mbaazi, bali na mazao mengine jamii ya mikunde,” alisema na kuongeza:

“Mwekezaji amekusudia kuwasaidia Watanzania, kiwanda kina thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 30, asingeweza kuwekeza hivi kama hajui anafanya nini:

Samia alisema hayo akiwa katika  Kiwanda cha Mahashree, na kupongeza asilimia 40 ya ajira kutolewa kwa wanawake.

Aidha, alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupotea kwa mazao ya kilimo, hivyo uwapo wa viwanda hivyo kutasaidia sana kukabiliana na tatizo hilo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema kuanzishwa kwa viwanda vingi kunaongeza uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima, na kwamba uwapo wa reli ya kisasa, umeme mkubwa na wa uhakika unadhihirisha uhakika wa serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Sadiq Murad, aliwahimiza wenye viwanda kuzingatia utunzaji wa mazingira, hasa ikizingatiwa kuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha kuchakata mpunga na kuzalisha mchele, Basheigha Haroun, alisema kiwanda hicho kitagharimu dola milioni 20 na kina uwezo wa kuzalisha na kuchakata tani 600 za mpunga kwa siku kwa awamu mbili, kwa kuanza na tani 300.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Mahashree, Malick Mahashree, alisena  wameshapata masoko ya bidhaa watakazozalisha katika nchi mbalimbali duniani ikiwamo China, India na Ujerumani na wataendesha shughuli zao kwa mfumo wa mikataba, kurahisisha mikopo na kusimamia masuala ya mbolea, na watazingatia pia ulimaji wa kilimo hai.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen, alisema Mkoa wa Morogoro umeanzisha viwanda vipya zaidi ya 3,000 vikiwamo viwanda vidogo 302 na vikubwa 20, vya kati na vidogo kabisa.

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, aliahidi wizara yake itaendelea kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi kuhakikisha shughuli za uzalishaji na uendeshaji wa viwanda zinafanikiwa ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, shule, hospitali na vituo vya afya.

 

Na Idda Mushi na Christina Haule