Nanenane ilete uwekezaji zaidi

09Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
 Nanenane ilete uwekezaji zaidi

NANENANE ilihitimishwa jana, lakini jukumu la kuendeleza kilimo, ufugaji na uvuvi ndiyo kwanza linaanza.

Maadhimisho hayo ya Nanenane yameendelea kutudhihirishia kuwa kilimo si tu kuwa ni mhimili wa uchumi bali pia ni msingi wa afya ya Watanzania, hivyo kunahitajika uwekezaji zaidi kwenye kilimo.

Bajeti ya kilimo inayopangwa iakisi ukweli kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa na kama ulivyo uti wa mgongo wa binadamu hakuna anyeruhusiwa kuuchezea.

Tunasisitiza kuwa ni lazima kuwekeza zaidi kwenye kilimo kwa kuwa wakulima wetu, wavuvi na wafugaji wametambua kuwa japo kwa miaka mingi kilimo hakikuhusishwa na biashara, leo wamejielewa na kufahamu kuwa kilimo ni biashara. Kujitambua huko ndiko kunakouhitaji zaidi mkono wa serikali.

Aidha, pamoja na kazi hiyo kufanywa na serikali kupitia maonyesho hayo ambayo hufanywa kitaifa, kikanda na kiwilaya kwenye maeneo mbalimbali nchini, uwekezaji wa kukiboresha na kukiimarisha kilimo unahitajika zaidi.

Hata hivyo, tunazipongeza taasisi za utafiti, masoko na uhamasishaji kwa kuwafungua wakulima, wavuvi na wafugaji macho na ambao sasa wametambua kuwa zamani kazi yao iliishia shambani na masuala mengine yangefanywa na ngazi nyingine za kiuchumi.

Ndiyo maana kupitia hamasa mbalimbali kama ilivyoonekana kwenye maonyesho hayo imethibitika kuwa wakati huu wakulima wanashindana miongoni mwao na wameanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao yao badala ya kuyatoa shambani, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kazi kubwa inayofanywa na serikali na wadau imetambulisha ukweli huo kuwa zama hizi kilimo ni biashara tena ni jukumu lenye tija zaidi duniani kwa kuwa ndicho chanzo cha chakula ambacho kila binadamu anakihitaji hivyo serikali imewahusisha na wavuvi na ufugaji tena kuwapa nafasi wazalishaji hao ili kuwa na uwanja mpana zaidi katika kuendesha shughuli zao.

Wakati Nanenane ikihitimishwa leo tunawapongeza wakulima na kuwatia moyo kuwa ndiyo tegemeo la kupatikana kwa chakula, malighafi kwa viwanda vya Tanzania na kwa ujumla ndicho kinachotegemewa kwenye kuusukuma uchumi wa nchi.

Ikumbukwe kuwa serikali inapolenga kuanzisha viwanda ni wazi kuwa vingi vitategemea moja kwa moja malighafi kama maziwa, nyama, nafaka, pamba, miwa na mbegu za mafuta ili kuzalisha bidhaa muhimu za viwandani. Ndiyo maana inahitajika kuwekeza zaidi.

Aidha, kutokana na kusinyaa kwa soko la ajira rasmi, kilimo leo ni ajira si tu kwa wakulima bali pia kwa mamilioni ya Watanzania wakiwamo vijana na wazee. Hivyo ikihitaji serikali kuwa karibu zaidi na sekta hii.

Kwenye sekta ndiyo ndiko wanakoajiriwa madereva wa malori, wauzaji sokoni, ndiyo mhimili wa hoteli za nyota tano na viwanda mbalimbali ambavyo vimeunganishwa na kilimo, ufugaji na uvuvi.

Tunaungana na kauli ya serikali kuanzia Tanzania ilipopata Uhuru hadi leo inayosisitiza kuwa kilimo ni mhimili na ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Kwa vile mazao kama kahawa, chai, korosho, ngozi, tumbaku, samaki na viungo vya aina mbalimbali vimeendelea kuwa chanzo cha fedha za kigeni.

Pamoja na kuwa mhimili wa uchumi tungependa kuongeza kuwa kilimo ndiyo mhimili wa afya ya Mtanzania.

Hii ni kwa sababu kutoka shambani, baharini na kwenye zizi la mfugaji kuna uhakika wa vyakula, kuanzia nyama, mboga, matunda, samaki na nafaka zinazoliwa na kuwapa wananchi afya.

Ndiyo maana tunaona kuwa serikali iongeze zaidi nguvu kwenye kilimo kwa kubuni teknolojia nyepesi, rahisi ili kukiboresha zaidi.

Habari Kubwa