Bodaboda tumieni vijiwe vyema staili hii ya uchumi

09Aug 2019
Yasmine Protace
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bodaboda tumieni vijiwe vyema staili hii ya uchumi

KATIKA hili naomba nianze kuwa mtaaluma wa lugha kwa kuweka sawa nadharia yangu katika lugha, ili kuweka sawa msingi wa hoja tuelezane vizuri.

Nikipitia msingi huo, nianze kutoa maana ya kijiwe kwamba ni kitu gani? Niseme ni mkusanyiko wa watu wengi wanaojishughulisha na yote ya kuwaongezea kipato.

Vivyo hivyo, kijiwe ni mahali watu wanajikusanya na kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu.

Hivyo mtu unapopita mitaani ni kawaida kukuta watu wamekaa katika ama mikusanyiko au aina fulani ya makundi katika sura ambayo yana malengo ya pamoja.

Niseme ni neno lililozoeleka kutamkwa na watu wanapowaona wenzao wamekusanyika katika maeneo hayo.

Katika hilo, nianze kuzungumzia maisha ya biashara za pikipiki aina ya bodaboda, kwamba ninaposema kijiwe cha bodaboda, ni ile sehemu ambayo bodaboda hujikusanya kwa kawaida wastani zaidi ya 10, kwa ajili ya kufanya biashara zao.

Vipo vijiwe ambayo vinamilikiwa na watu na wamekuwa wakipata fedha kupitia vijiwe hivyo. Baadhi ni kwamba, bodaboda wamejisajili na kuzipa majina, ili waweze kunufaika na mikopo ikiwamo kutambulika.

Hivi karibuni, madereva wa bodaboda wawanaounda umoja uitwao ‘Bodaboda Group’ eneo la  Mlimani City Jijini Dar es Salaam, wamezindua umoja wao ambao wanalenga kujiinua kiuchumi. 

Mwenyekiti wao, Jafari Yahaya, anasema kikundi chao kilianzishwa tangu mwaka 2014 na kupata usajili mwaka jana  na hadi sasa kina wanachama 25 waliofanikiwa kufungua akaunti na kuhifadhi zaidi ya shilingi milioni moja. 

Anasema kufunguliwa kwa umoja huo, kumewasaidia kujenga mshikamano na kusaidiana katika shida, wakiishi katika mfumo kila mwana kikundi kwa siku anachangia zaidi cha Sh. 1000. Ni pesa anayopatiwa mwana kikundi anayeumwa. 

Yahaya anasema, kuwapo matukio ya ajali katika  sehemu za kazi, kikundi chao kimehakikisha kila mwana kikundi kimenufaika na kadi za matibabu, kwa maana ya  bima za afya.

Anasema katika orodha hiyo, kila mwanachama kwa wiki anachangia fedha Sh. 20,000 zinazotunzwa benki. Anataja changamoto yao ni kwamba, madereva wa bodaboda hawaruhusiwi kufika maeneo ya mijini na mazingira muhimu ya biashara kama vyuo vikuu jirani.

Ombi lake ni kwamba, serikali isiwazuie kwa sababu umoja huo una vitambulisho vyao maalum na anapaza sauti kwa wafadhili wajitokeze kuwasaidia, wapate eneo ambalo watakalolitumia kama shamba, kwa ajili ya kuwekeza shughuli zao za maendeleo.

Anataja changamoto nyingine wanayokumbana nayo, ni baadhi yao kutomiliki bodaboda, hivyo ni kilio kingine kinaviendea vyombo vya kuwakopesha. 

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makongo, jijini Dar es Salaam Husina Hondo, anaahidi kuzifikisha changamoto hizo kwa mamlaka za juu, ili kuwapatia ufafanuzi mkubwa ambao ndio watazitolea majibu.

Mtendaji huyo amekipongeza kikundi hicho na kuvitaka vingine viige mfano wa kuweka akiba na kuwa na kadi za bima.Alisema vikundi vikiwapo ni rahisi kupatiwa mikopo inayotolewa na serikali.

Habari Kubwa