Wagonjwa wa figo SADC kupokelewa

09Aug 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wagonjwa wa figo SADC kupokelewa

TANZANIA inatarajiwa kuongeza kupokea idadi ya wagonjwa watakaoletwa kutibiwa nchini kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), baada ya kufanikiwa kuboresha na kuanzisha huduma za kisasa ikiwamo upandikizaji wa figo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizungumza jana kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Alibainisha kuwa kupitia maonyesho hayo, sekta ya afya imepata fursa ya kuonyesha kuwa Tanzania sasa inakuwa nchi ya utalii wa kimatibabu na kupitia huduma za kisasa zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

Alitaja huduma hizo ni upandikizwaji wa figo, vifaa vya kusikia kwa watoto na kutibu kwa kutumia radioloji unaofanywa kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. 

Alisema huduma hizo awali zilikuwa hazipatikani nchini wala katika nchi za SADC, zaidi ya Afrika Kusini inayotoa upandikizaji wa figo, lakini nyingine hazijaanza, hivyo Tanzania inapata fursa ya kupokea wagonjwa kutoka nchi wanachama wa SADC. 

Alisema hatua hiyo inajenga mazingira kwa wanajumuiya ya SADC kutokuwa na haja ya kupeleka wagonjwa wao kutibiwa nje ya nchi za jumuiya hiyo, badala yake watapokelewa na kutibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). 

Awali, alibainisha Wizara ya Afya inaamini mkutano wa SADC utaongeza  idadi ya wagonjwa wanaopokelewa kutoka Jumuiya hiyo ambayo ilikuwa ni  wagonjwa 24 kila mwezi, kutoka nchi za SADC na hasa nchi ya Jamhuri ya  Kidemokrasi ya Congo (DRC), Comoro na Malawi. 

Waziri Ummy alisema kupitia Mkutano wa SADC unaofanyika nchini kuna mambo mengi ambayo Tanzania itanufaika, miongoni mwa hayo ni huduma za kisasa za afya zinazotolewa nchini kwa sasa. 

Aliyasema hayo baada ya kutembelea maonyesho ya viwanda ya SADC na  alipita kujionea mabanda ya sekta ya afya ikiwamo la Hospitali ya Taifa  ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na  Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kusema kuna huduma za tiba ya  kisasa zinazotolewa katika taasisi hizo. 

"Katika maeneo haya ya maonyesho tumejipanga vizuri kutoa huduma ya tiba ya dharura, kuna ambulance 22, pamoja na vyumba maalum vilivyotengwa kwa huduma hizo kwa mtu atakayepata matatizo ya kiafya katika mkutano huu," alisema. 

Habari Kubwa