12 matatani umiliki kampuni za kubadili fedha bila kibali

09Aug 2019
Dege Masoli
TANGA
Nipashe
12 matatani umiliki kampuni za kubadili fedha bila kibali

JESHI la Polisi mkoani Tanga, linawashikilia wafanyabiashara 12 kwa tuhuma za kumiliki kampuni za kubadilisha fedha bila kufuata taratibu za kisheria.Kwa mujibu wa sheria ya fedha, wanatakiwa kuwa na kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Leons Rwegasira, alisema jana kuwa wafanyabiashara hao walikamatwa kwenye operesheni ya kushtukiza iliyofanywa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vya usalama wakiwamo maofisa wa Hazina.

Alieleza kuwa mbali na watu hao, pia kuna fedha za Kitanzania na za kigeni walizokamatwa nazo pamoja na madini, kemikali na noti bandia.Kwa mujibu wa Kamanda huyo, fedha za Kitanzania walizokutwa nazo ni Sh. milioni 63.3, na fedha za kigeni na thamani yake kwa fedha ya Kitanznaia kwa viwango vya kubadilishia fedha siku ya jana kwa mujibu wa Conveter, ni Dola za Marekani 65,961 (sawa na Sh. milioni 151.7), fedha za Kenya Sh. 236,549 (sawa na Sh. milioni 5.3).

Nyingine ni Paundi 400 (sawa na Sh. milioni 1.1) na Euro 270 (sawa na Sh. 694,884), Rupia zipatazo 1,349, fedha ya Afrika Kusini Rand 1,020 (sawa na Sh.154,810), fedha ya Oman Rial 521 (sawa na Sh.milioni 3.1) na Uganda ni Sh 2000 (sawa na Sh. 1,246).

Aidha, alieleza tuhuma nyingine zinazowakabili ni kukutwa na madini na kemikali ambazo hazijabainika ni za aina gani na matumizi yake. Kamanda huyo alisema pia watuhumiwa hao wamekutwa na fedha bandia. 

Aidha, aliwataka watu wanaotaka kufanya biashara hiyo kufuata taratibu za kisheria ikiwamo kuwa na vibali kutoka BoT ili kuepukana na kuingia kwenye makosa ambayo yatawafanya kuharibu mfumo wa maisha yao. 

“Tunataka watu wafuate sheria inayowataka kusajiri kampuni zao BoT na kuingia kwenye utaratibu wa kulipa kodi ya serikali, vinginevyo hawatakuwa salama kwani Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote atakaekwenda kinyume cha sheria,” alisisitiza Rwegasira.

Habari Kubwa