Mikopo elimu ya juu inavyogeuka shubiri

09Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
 Mikopo elimu ya juu inavyogeuka shubiri

BAADHI ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wamelalamika kuhusu kile wanachokiita uonevu katika marejesho ya mikopo hiyo.

Miongoni mwa masharti yanayolalamikiwa na wanufaika wa mikopo hiyo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ni deni kuongezeka kwa asilimia sita kila mwaka kunakosababisha ugumu wa kumaliza kulilipa.

Takwimu za HESLB zinaonesha kati ya Watanzania 479,779 waliopatiwa mikopo hiyo tangu serikali ilipoanza kuitoa mwaka 1994, ni wanufaika 11,214 (asilimia 2.3) waliofanikiwa kumaliza kulipa madeni yao.

Akiwa mjini Shinyanga juzi, Kashinje Emmanuel (33), mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, aliiambia Nipashe kuwa alitarajia kumaliza kulipa mkopo wake ndani ya kipindi cha miaka 18, lakini ameshangaa kuona deni linaongezeka kila mwaka ilhali ameshaanza kulilipa tangu mwaka 2015.

"Mimi nilisoma Udom (Chuo Kikuu cha Dodoma) 2009-2012. Bodi (HESLB) ilinipa jumla ya Sh. milioni 8.04, wakati naanza kulipa mwaka 2015, deni lilikuwa limefika Sh. milioni 12 maana tayari walikuwa wameshanipiga penalti na tozo nyingine.

"Nikaanza kulipa kwa kukatwa Sh. 56,000 kila mwezi kwenye mshahara wangu na nikajipa matumaini kwamba deni lingemalizika ndani ya miaka 18.

"Kilichonishangaza ni kwamba licha ya kuanza kulipa, deni halipungui kwa kiasi kikubwa, linapungua kidogo sana, (HESLB) wanaongeza asilimia sita kila mwaka, ni ngumu kwangu kulimaliza kama mshahara wangu utaendelea kuwa hivi," alisema mwalimu huyo wa Shule ya Sekondari Com iliyoko mjini Shinyanga.

Mnufaika mwingine wa mikopo hiyo, Fortunata Ntwale, aliiambia Nipashe jijini Dar es Salaam jana kuwa naye anaumizwa na kuongezeka kwa deni hilo kwa asilimia sita kila mwaka pamoja na makato makubwa yanayofanyika katika urejeshaji wa mkopo baada ya Bunge kupitisha marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Novemba 2016, Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2016, ambao pamoja na mambo mengine, ulipendekeza kurekebisha Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili mnufaika wa mkopo arejeshe mkopo kwa makato si chini ya asilimia 15 ya mshahara wake wa kila mwezi badala ya asilimia nane ya awali.

"Mimi nilisoma sheria pale UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) 2011-2014, nimeanza kurejesha mkopo mwaka huu. Kwa kweli makato ya asilimia 15 ya mshahara ni makubwa sana. Anayeomba mkopo huo kwa sasa inabidi afikiri mara mbili maana hata ajira zenyewe ni shida.

"Kibaya zaidi, unapigwa penalti kama hutalipa deni mapema baada ya kuhitimu masomo. Hata ukiwahi kuanza kulipa, bado deni linaongezeka kwa asilimia sita kila mwaka, na kuna makato mengine ya asilimia moja ambayo bodi inatukata kwa ada ya uendeshaji ilhali watumishi wake wameajiriwa ili wafanye kazi hiyo.

"Nafikiri kuna haja kuiangalia upya sheria hii, inatuumiza wananchi. Kwenye mshahara ukikatwa bima ya afya, kodi ya serikali, NSSF na Bodi ya Mikopo unabakiwa na fedha kidogo sana, inavunja moyo."Penalti imetukumba watu ambao tulipohitimu chuo, hatukupata kazi, tungerejesha mikopo kupitia vyanzo vipi? Huu ni mkopo wa serikali kwa wananchi wake, siyo wa kibiashara, ulenge zaidi kusaidia na siyo kukomoa," Ntwale alishauri.

Akiwa mjini Mtwara jana, mnufaika mwingine wa mikopo hiyo, Nzumi Malendeja, aliambia Nipashe kuwa kuna haja serikali kufanya marekebisho mengine kwenye Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili wanufaika walipe kiasi kilekile walichokopeshwa badala ya deni kuongezeka kwa asilimia sita kila mwaka.

Malendeja alisema alinufaika na mkopo wa HESLB kwa kupatiwa Sh. milioni nane alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 na alianza kurejesha mkopo huo Machi mwaka huu baada ya kuajiriwa na Aga Khan Foundation, deni likiwa limefika Sh. milioni 22. "Ninaona ni deni ambalo haliishi kwa sababu linaongezeka kila mwaka, nafikiri wanufaika tulipe lakini kusiwe na ongezeko la asilimia sita kila mwaka.

"Pia, makato ya asilimia 15 ni makubwa mno, yanapunguza hata uwezo wa mnufaika kukopeshwa na taasisi nyingine za kifedha kwa sababu tayari anakuwa na mzigo wa kulipa deni hilo la HESLB, NSSF na kodi ya serikali. "Ninaamini makato haya makubwa ndiyo yanayotengeneza mazingira ya wanufaika kutafuta mbinu za kukwepa kurejesha fedha walizopewa," Malendeja alisema.

Kifungu 7.2.1.1 cha Mwongozo wa HESLB wa Utoaji Mikopo na Ruzuku kwa Wanafunzi kinabainisha kuwa, ili kuhakikisha mfuko wa ukopeshaji unakuwa endelevu, mnufaika wa mkopo wa bodi hiyo atalipa tozo ya kulinda thamani ya fedha ambayo itakatwa asilimia sita kwa mwaka tangu tarehe mnufaika aliyoanza kupokea mkopo.Vilevile, katika kifungu 7.2.1.2 cha mwongozo wake huo, HESLB inaeleza kuwa itakata asilimia moja ya ada ya uendeshaji kwa mwanafunzi mnufaika.

Pia, katika kifungu 7.2.1.3 cha mwongozo huo, inaelezwa kuwa ikiwa mnufaika atashindwa kulipa mkopo baada ya kipindi cha neema cha miezi 24 baada ya kuhitimu masomo yake, ataongezwa makato ya adhabu ya asilimia 10.

KAULI YA HESLB

Akizungumza na Nipashe kwenye ofisi ya HESLB zilizoko Mwenge jijini Dar es Salaam juzi, Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole, alisema changamoto ya deni kuongezeka na wanufaika kushindwa kumaliza kulilipa inatokana na wengi wao kuchelewa kuanza kulipa, hivyo kukumbana na adhabu.Alisema ili mnufaika aweze kumaliza deni lake kwa wakati na kutoonekana linaongezeka kila mwaka, anatakiwa kuanza kulipa kwa wakati uliopangwa na bodi.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Ngole alisema kwa mnufaika aliyepewa mkopo wa Sh. milioni 6.12, kama atalipa kwa wakati (bila penalti), akiwa na mshahara wa kati ya Sh. 700,000 na 750,000, atakatwa Sh. 109,000 kila mwezi na atamaliza kulipa deni lake la Sh. milioni 7.201 (ongezeko la Sh. milioni 1.081) katika kipindi cha miaka mitano na miezi saba.

Kwa mnufaika aliyepata mkopo wa Sh. milioni 13, Ngole alisema deni lake litakuwa Sh. milioni 17.082 na kama atalipa bila penalti, mshahara wake ukiwa kati ya Sh. milioni moja na milioni 1.4, kila mwezi atakatwa Sh. 150,000 na atamaliza kulipa deni katika kipindi cha miaka tisa na miezi mitano.

Ngole pia alisema mnufaika aliyepewa Sh. milioni 20, atatakiwa kulipa Sh. milioni 26.516 kama hatapigwa penalti na atakamilisha kulipa deni lake katika kipindi cha miaka tisa na miezi minane ikiwa mshahara wake ni kati ya Sh. milioni 1.5 na milioni 1.9 kwa kukatwa Sh. 225,000 kila mwezi.

Meneja huyo pia alieleza kuwa mnufaika aliyekopeshwa Sh. milioni 50 atatakiwa kurejesha Sh. milioni 65.978 na kama atalipa kwa wakati kwa kukatwa kila mwezi asilimia 15 ya mshahara wa kuanzia Sh. milioni 3.8 (Sh. 570,000), deni lake litakamilika katika kipindi cha miaka tisa na miezi saba.

Ngole alibainisha mpaka sasa, ni wanufaika 11,214 waliofanikiwa kumaliza kulipa madeni yao. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 2.3 ya wanufaika wote 479,779 waliopewa mikopo yenye jumla ya Sh. trilioni 3.889 tangu serikali ilipoanza kuitoa mwaka 1994.

Alisema HESLB ipewe jukumu la kusimamia urejeshwaji wa mikopo hiyo mwaka 2007, wahitimu 11,214 waliofanikwa kumaliza madeni yao, wamelipa jumla ya Sh. bilioni 67.6 na kupewa vyeti.

Meneja huyo alisema jumla ya wahitimu 145,656 hawajaanza kulipa mikopo yao ya jumla ya Sh. bilioni 432.5 na wana zaidi ya miaka 10 tangu wahitimu masomo yao. Kiasi hicho cha fedha ni zaidi ya mikopo iliyotolewa na HESLB kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, katika mwaka huo wa fedha (2018/19), bodi hiyo ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 427 kwa wanafunzi 123,285. Kati yao, wa mwaka wa kwanza walikuwa 40,544 na wanaoendelea na masomo walikuwa 82,741.

Ngole alisema wahitimu 162,983 wanaendelea kurejesha mikopo yao kila mwaka na kwa mwaka jana walifanikiwa kukusanya Sh. bilioni 183 na mwaka huu wanatarajia kukusanya Sh. bilioni 221.

Alisema wanufaika wengine 123,329 ni wanafunzi ambao wanaendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini na hawajaanza kurejesha mikopo, hivyo kuwekwa kundi moja na wadaiwa wengine ambao wako katika kipindi cha neema cha miaka miwili baada ya kuhitimu.

"Jumla ya wahitimu 145,656 ambao tunawaita sugu, hawajawahi kurejesha mikopo yao hata kidogo, fedha ambazo zinafika Sh. bilioni 432.5. Tuna mikakati mbalimbali ya kuhakikisha tunawapata ili waanze kurejesha," Ngole alisema.

Meneja huyo aliitaja mikakati ya bodi hiyo kuhakikisha inawanasa wanufaika hao wa mikopo yake kuwa ni pamoja na kukutana na wadau wa kimkakati kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Chama cha Waajiri (ATE) na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kubadilishana taarifa za kuwabaini.Ngole pia alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wanufaika na waajiri kuhusu umuhimu wa kurejesha mikopo yao kwa wakati.Alisema bodi hiyo pia inafanya ziara za ukaguzi kwa waajiri kwa kupitia orodha ya malipo ya mishahara ya wafanyakazi wao.Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, Mwanasheria Frank Mushi aliwataka waombaji wa mikopo hiyo kutokimbilia kutia saini mkataba ya kupewa mkopo hadi pale wanapojiridhisha kuhusu masharti ya mkopo huo."Kibaya zaidi sheria za mikataba zinasema inapotokea mkataba umeandikwa na mkautia saini, wote mnakuwa mmefungwa na 'terms' (masharti) za ule mkataba."Kwa hiyo, lazima mwanafunzi anapotia saini aangalie kwa umakini masharti yaliyomo. Chochote kinachofanyika kama ni ongezeko la sita au nini, lazima atambue mapema."Lakini nafikiri sheria iangaliwe kama Bodi ya Mikopo ni taasisi inayofanya biashara au ipo na nia ya kuwasaidia wananchi hasa kipindi hiki ambacho kuna changamoto kubwa ya ajira," alisema. 

 

Habari Kubwa