Shein asafisha njia ya Kiswahili SADC

09Aug 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shein asafisha njia ya Kiswahili SADC

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuna haja Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za mawasiliano katika majukwaa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Amesema anaamini hatua hiyo itaimarisha umoja na mshikamano kwa wanachama wa jumuiya hiyo na kukuza shughuli za biashara na viwanda.

Dk. Shein aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifunga maadhimisho ya Maonyesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC.

“Historia inatuonyesha Kiswahili kimeweza kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja, licha ya kwamba Watanzania wanazo lugha tofauti za makabila mbalimbali.

"Kiswahili kimekuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa Afrika. Hivi sasa, Kiswahili kimerahisisha mawasiliano na kukuza biashara katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na tayari Umoja wa Afrika (AU) umekikubali Kiswahili kiwe ni lugha rasmi.

"Kwa hivyo, wazo la kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za SADC ni muhimu na vyema tukaungana katika kulifanyia kazi suala hili,” alisema.

Rais Shein pia alizitaka nchi za SADC kuendeleza viwanda, kununua na kuzipenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya jumuiya hiyo.

Alizitaka kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwatumia wataalamu wazawa na kuondokana na utegemezi wa wataalamu kutoka nje, sambamba na kujenga misingi imara ya kuendeleza teknolojia asilia.

“Kazi  iliyo mbele yetu sasa ni kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anaunga mkono utelekezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika vikao vilivyofanyika pamoja na mikakati ya serikali zetu zote ya kuendeleza viwanda kwa kununua na kuzipenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu wenyewe,” alisema.

Rais Shein alisema kwa kufanya hivyo ni kutafsiri kwa vitendo dhamira ya nchi za SADC kuunda umoja kwa ajili ya kuongeza fursa ya masoko na ajira.

Alisema nchi hizo zitaweza kuongeza masoko na ajira ikiwa  zitanunua bidhaa zinazozalishwa na viwanda kutoka jumuiya yao wenyewe na vinavyoendeshwa na wataalamu wazalendo.

Alisema nchi za SADC zinatakiwa kuongeza ubora wa bidhaa za viwandani ili ziweze kushindana na zile ambazo watu wengine hupenda kuzinunua.

Alisema kunapaswa kutengenezwa kwa bidhaa zenye ubora katika utengenezaji na ubunifu wa hali ya juu utakaoweza kuwavutia wanunuzi wengi.

Rais Shein pia alisema katika utafutaji wa masoko, nchi za SADC zinapaswa kuweka mkazo katika Technolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayotokana na utandawazi.

 

Gwamaka Alipipi na Beatrice Moses

Habari Kubwa