Waziri Mkuu ataka ripoti timu mawaziri wanane

09Aug 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri Mkuu ataka ripoti timu mawaziri wanane

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa, amewaagiza mawaziri wanane waliopewa kazi ya kutembelea maeneo yenye migogoro ya wakulima, wafugaji na wahifadhi, kukamilisha taarifa ili changamoto hiyo imalizwe mapema.

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana mkoani Simiyu katika maadhimisho ya kitaifa ya maonyesho ya Nanenane. “Pamoja na mafanikio kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, Sekta ya kilimo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ikiwamo ukame, milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mazao, teknolojia duni za kilimo na uhifadhi wa mazao na migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya wafugaji na wahifadhi,” alisema.

Majaliwa alisema serikali imeendelea kuzitatua changamoto hizo na kwamba migogoro kati ya wafugaji na mipaka ya hifadhi tayari imeifanyiwa kazi.“Tumeifanyia kazi kwa kuteua timu ya mawaziri wanane kwenye sekta zinazogusa maeneo hayo kuyatembelea yote yanayolalamikiwa, ninawahakikishia migogoro hiyo inafanyiwa kazi. “Wanakamilisha taarifa, tunataka kuimaliza kabisa. Wito wangu kwa mawaziri mliohusika kwenye hili, harakisheni mchakato huo ili wakulima na wafugaji wanaoishi kandokando ya hifadhi wajue hatima ya kazi zao, nataka tuwaeleze mipaka ipo wapi," aliagiza.

Alisema lengo ni kuona uwezekano wa baadhi ya hifadhi kupunguzwa ukubwa wake pale ambako wanaona hakuna tija ili wananchi waendeleze maeneo hayo kwa shughuli za ufugaji na kilimo. Kuhusu zao la pamba, Majaliwa alisema serikali kupitia Benki Kuu (BoT) imewaunganisha wanunuzi na wenye benki ili waweze kupata fedha za kununua pamba kutoka kwa wakulima.

Alisema soko la pamba limekumbwa na changamoto ya ununuzi lakini kuanzia Jumatatu, wakulima watakuwa wanafurahia matunda ya jasho lao.Majaliwa alisema baadhi ya wanunuzi wameshakwenda kwenye vituo vya ununuzi ili kuinunua pamba na serikali imeanza kupata taarifa za vituo kulipa pamba iliyokuwa vituoni kwanza. Kuhusu sekta ya uvuvi, Majaliwa alimwagiza waziri mwenye dhamana kuhakikisha elimu zaidi inatolewa kwa wavuvi ili kuondoa migongano kati yao na serikali na iandae mpango maalum wa aina ya nyavu zinazotakiwa kutumiwa wakati wa kuvua.

Habari Kubwa