Fatma Karume afunguka udukuzi wa mawasiliano

09Aug 2019
Enock Charles
DAR ES SALAAM
Nipashe
 Fatma Karume afunguka udukuzi wa mawasiliano

RAIS mstaafu wa Chama cha Wanasheria (TLS) na wakili wa kujitegemea, Fatma Karume, amezishauri kampuni za mawasiliano ya simu nchini kuwalinda watumiaji wao dhidi ya udukuzi wa taarifa binafsi.

RAIS mstaafu wa Chama cha Wanasheria (TLS) na wakili wa kujitegemea, Fatma Karume

Amesema kampuni hizo zinao wajibu wa kuchukua hatua madhubuti pale inapobainika taarifa za mteja kudukuliwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

"Kampuni za simu zina wajibu wa kuchukua hatua kulinda wateja wao kwa kuwa wao wana mkataba na wateja na madhara ya udukuzi si kwa wadukuaji, bali ni kwa kampuni na wateja," Fatma alisema katika mahojiano na moja ya vituo vya televisioni jijini Dar es Salaam juzi.

Wakili huyo alisema si jambo jema taarifa binafsi za watu kuwekwa hadharani na kama italazimika kufanyika hivyo, basi ni muhimu pakawapo na utaratibu wa kisheria ili kuepuka kukiukwa kwa haki za msingi za wateja. "Tukumbuke huu udukuzi ulianza na nani? Unakumbuka (Freeman) Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema) 'telephone conversation' (mawasiliano ya simu) na Wema Sepetu, ulianza pale Watanzania tukawa tunacheka hee hee hee. "Tunamcheka Mbowe, wakatoka pale wakamwingilia Nape (Nnauye-Mbunge wa Mtama) na (Abdulrahman) Kinana (Katibu Mkuu mstaafu wa CCM).

"Walipomaliza na hapo, wakaingilia January (Makamba) na babaake (Yusuph Makamba), walipomaliza wakaja kwa (Benard) Membe na mtu mwingine. “Unasikiliza January Makamba anaongea na Yusuph Makamba, mtoto na baba, hii siyo sawa hata kidogo," Fatma alisema.

Wakili huyo aliongeza kuwa ni muhimu nchi kutunga sheria itakayodhibiti udukuzi wa mawasiliano ya watumiaji wa mitandao ya simu isipokuwa kwa matakwa maalum ya kisheria na sababu zinazojitosheleza za kufanya udukuzi huo.

Hivi karibuni, kulivuja mawasiliano ya simu yaliyodaiwa kuwa na sauti za viongozi wastaafu wa CCM. Mawasiliano hayo yalisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, huku mmoja wao akikiri sauti iliyodukuliwa ni yake na anawafahamu waliofanya hivyo ingawa hawezi kuwataja kwa kile alichoeleza kuwa ni sababu za kimaadili.

Kuvuja kwa sauti hizo pia kuliwaibua watetezi wa haki za binadamu ambao waliitaka serikali kutunga sheria kulinda taarifa binafsi ili kuepusha ukiukwaji wa haki ya faragha.

Ibara ya 16 ya Katiba ya Tanzania inaeleza kuwa kila mtu anastahili kuheshimiwa na faragha yake kulindwa, na mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria kuhusu hali hii namna na kiasi ambacho haki ya mtu ya faragha yaweza kuingiliwa bila ya kuathiri ibara hiyo.

Habari Kubwa