Lukuvi awasimamisha kazi maofisa 183 ardhi

09Aug 2019
Joseph Mwendapole
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lukuvi awasimamisha kazi maofisa 183 ardhi

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amepitisha fagio la chuma wizarani kwake baada ya kuagiza kusimamishwa kazi kwa maofisa 183 wa wizara hiyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Maofisa hao wanatuhumiwa  kuingilia mfumo wa kukadiria na kukusanya kodi ya pango la ardhi kinyume na taratibu na kusababisha upotevu wa mapato ya serikali.

Katika taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa juzi usiku, Lukuvi alimwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwasilisha majina ya maofisa hao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili uchunguzi uanze mara moja.

Wengi wa waliotumbuliwa ni maofisa ardhi wa wilaya, maofisa ardhi wasaidizi wa wilaya, wahasibu, wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT), wathamini wa ardhi, makatibu muhtasi, maofisa ardhi wateule na watunza kumbukumbu.

Katika sakata hilo wengine waliokumbwa ni watunza fedha na maofisa kutoka makao makuu ya wizara hiyo.

Alipoulizwa kama majina hayo yameshawasilishwa Takukuru, Meneja Mawasiliano wa taasisi hiyo, Doreen Kapwani, alisema jana ilikuwa sikukuu hivyo ni vyema atafutwe leo kwa ajili ya ufafanuzi.

"Leo ni sikukuu kwa hiyo suala hilo hakuna wa kufuatilia ila kesho ni siku ya kazi hivyo ukinitafuta nitakupa maelezo kwa sababu hata hiyo taarifa unayosema sijaiona," alisema.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani, kujua kama majina hayo yameshawasilishwa mezani kwake ziligonga mwamba kwani simu yake ilikuwa inaita muda wote bila kupokelewa.