Mirerani waipinga kulipa kodi TRA

10Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
MANYARA
Nipashe
Mirerani waipinga kulipa kodi TRA

WAMILIKI na wachimbaji wa madini ya tanzanite wa Mirerani wilayani Simanjiro, wameshikwa na sintofahamu baada ya Serikali kuanza kuwadai kodi ya ajira inayotokana na mishahara wanayolipa wafanyakazi.

Mshangao huo umeibuka baada ya Mamlaka ya Mapato  (TRA) mkoani wa  Manyara, kuweka matangazo migodini ya kudai  malimbikizo ya kodi za ajira kwa wachimbaji wa madini.

Wachimbaji hao walidai kuwa tangazo hilo limewaathiri wachimbaji wengi na kuwaacha vinywa wazi kwani suala la ajira kwenye machimbo hayo halipo.

Wakizungumza jana wachimbaji hao walisema Rais John Magufuli, alikutana na wadau wa madini mwanzoni mwa mwaka huu na akaagiza kodi zisizo rafiki na wachimbaji ziondolewe ila wanashangazwa na tangazo hilo la TRA.

Mchimbaji Ally Seif, alisema suala la kulipa mishahara kwa wafanyakazi wa madini ya tanzanite halipo hivyo kuagiza walipe kodi ya ajira ni kuwaonea.

"Sisi hatulipani mishahara kila mwezi huku kwetu katika madini tunalipana mara baada ya kupata uzalishaji kama hujapata madini utawalipaje hadi utoe kodi ya ajira," alihoji Seif.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (Tawoma), Rachel Njau, alisema wachimbaji wanapaswa kutulia kwenye kipindi hiki ambacho tangazo hilo limetolewa.

Mchimbaji Michael Mekasi akitoa ya moyoni, alisema wachimbaji walielezwa na Rais Magufuli kuwa kodi zisizo na mashiko zitaondolewa na ndicho wanachoamini hivyo suala la kuambiwa walipe kodi ya ajira ni jambo geni.

Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima, alisema Mirerani ni eneo tengefu la madini, hivyo endapo TRA wanajambo  wanapaswa kushirikisha tume ya madini.

Ntalima alisema hivi sasa madini ya tanzanite yamezungukwa na ukuta endapo kuna taasisi au mamlaka inayotaka kufanya jambo lake ni vyema kushirikishana ili kuondoa migogoro na migongano.

Hata hivyo, Meneja wa Mamlaka ya Mapato  Mkoa wa Manyara, John Mwigula, alisema wachimbaji wanaolipwa mishahara wanapaswa kulipiwa kodi ya ajira kwa mujibu wa sheria.

"Huyo mchimba madini  ambaye atakuwa anafanya kazi kwako kwa miaka mitano au zaidi atakuwa anaishije na kujikimu kwa namna gani bila malipo? Hayo makubaliano mnayosema ni kulipana baada ya madini kutoka ni ya namna gani," alihoji Mwigula.

Habari Kubwa