Kaskazini yasifika kuzalisha   ng’ombe wa kilo 1,000

10Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Kaskazini yasifika kuzalisha   ng’ombe wa kilo 1,000

KANDA ya Kaskazini imemwagiwa sifa kemkem kwa kutekeleza malengo ya serikali ya kuwasaidia wafugaji na wakulima kuboresha kilimo na mifugo.

Hayo yalijiri baada ya kuzalisha ng’ombe bora mwenye uzito wa tani moja (kilo 1000) na kuonekana kwenye maonyesho hayo.

Akizungumza jana jijini Arusha wakati akifunga maonyesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Themi Njiro, yaliyoadhimishwa kama Kanda ya Kaskazini, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, alisema upatikanaji wa ng’ombe bora ni mafanikio ya sera ya  kuanzisha viwanda vya nyama na maziwa.

Alisema kikubwa kilichomfurahisha ni kwamba ng’ombe hao wanapatikana kwenye taasisi binafsi tofauti na miaka ya nyuma ilikuwa ikipatikana kwenye hifadhi za taifa za malisho ya serikali na taasisi za umma.

“Hii inamaana kuwa wananchi wote wameshaelewa nia ya serikali ya kukataa Tanzania kuitwa maskini wakati ni tajiri wa rasilimali mbalimbali, sababu tunapokuwa na mifugo bora tunapata nyama, maziwa na bidhaa bora na pia kilimo kikiwa bora tunaondokana na njaa na tunaweza kuuza hata nje ya nchi, lakini tunaweza kuanzisha viwanda vyetu sababu malighafi tunazo” alisema Ulega.

Aidha, aliziagiza halmashauri nchini kuweka mipango mikakati ya kuwezesha maofisa ugani kutoa elimu kwa wakulima, wavuvi na wafugaji vijijini, ili wazalishe bidhaa zenye tija na kuwashindanisha bidhaa wanazozalisha ili kuleta ushindani zaidi wa uzalishaji bora.

Akitoa mfano alisema kama kanda hiyo kila mkoa imejitahidi kuhakikisha inakuwa na kiwanda cha kuongeza thamani ya mifugo,uvuvi na kilimo na hiyo inasaidia wananchi kuondokana na tatizo la soko la bidhaa zao na kujikwamua kiuchumi.

Pia alisema amekubaliana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo la kuomba waonyeshaji waongezewe siku za kuonyesha bidhaa zao na kutoa elimu kwa wafugaji na wakulima hadi Jumatatu Agosti 12 mwaka huu.

“Nafahamu maonyesho haya yalikuwa siku za kazi, hivyo wengi hawakupata nafasi ya kuja katika maonyesho haya, sasa nakubali kuwaongeza muwepo hadi jumatau ili siku za mapumziko waje wengi zaidi kuvuna elimu mnayotoa, japo nayafunga leo ila endeleeni kuwapo hapa,”alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alisema anaamini maonyesho hayo yataongeza uzalishaji kwa mkoa wao, kwani kwa mwaka huu 2018/19 wana upungufu wa chakula tani 50,000 ili kufikia mahitaji yao ya tani 420,000 ya chakula.

Habari Kubwa