Watafiti waja na wadudu wala wadudu waharibifu

10Aug 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Watafiti waja na wadudu wala wadudu waharibifu

UTAFITI wa kibaiolojia uliofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRi), umebaini aina nne za wadudu wanaoweza kutumika kula wadudu wenzao waharibifu wa zao hilo.

Imeelezwa kuwa wadudu hao wana uwezo mkubwa wa kuangamiza kizazi cha wadudu waharibifu wa zao la kahawa likiwa shambani na kusaidia uzalishaji wake kuwa wenye tija.

Nipashe lilidokezwa jana na Mtafiti wa Wadudu wa TACRi, Fedrick Magina, kuhusu uthibitisho huo wa kisayansi wa ugunduzi wa wadudu hao.

“Ni kweli tumegundua aina mpya nne za wadudu ambao tunaweza kuwatumia kuangamiza wadudu wanaoshambulia zao la kahawa, tunaamini kwamba wadudu hao watakuwa suluhisho la magonjwa ya kahawa yanayosababishwa na uvamizi wa wadudu tuliowazoea.

“Hii inaweza kuwa ni mafanikio makubwa na habari njema kwa wakulima wa kahawa nchini, majibu ya kisayansi yanathibitisha kwamba wadudu hao wanaowashambulia na kuwala wadudu wenzao waharibifu wa zao la kahawa likiwa shambani, wataongeza zaidi tija na ufanisi katika uzalishaji na uwekezaji wa kilimo cha kahawa," alisema.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo wa wadudu, aina mpya ya wadudu waliogunduliwa wamepewa jina la dudukobe.

Alipoulizwa kuhusu namna idara hiyo ndani ya TACRi ilivyojipanga kuzalisha wadudu hao kwa wingi ili kuwasaidia wakulima wa kahawa kukabiliana na wadudu waharibifu, Magina alisema changamoto inayojitokeza kwa sasa ni namna ya kuwazalisha kwa wingi na kuwasambaza kwa wakulima.

Kwa ugunduzi huo, baadhi ya wakulima wa kahawa akiwamo Athanas Leba waliokuwa katika maadhimisho ya 26 ya wakulima wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, wameeleza kufurahishwa kwao na ujio huo wa majibu ya kitafiti ya kukabiliana na magonjwa ya zao hilo. 

"Ni vizuri wataalamu wetu wamekuja na majibu ya changamoto hii, lakini pamoja na kuipongeza TACRi kwa hatua hiyo, bado kiu yetu nyingine kubwa ni bei ya soko hasa kwa kahawa ghafi tunayoizalisha. Kimsingi haturidhishwi na bei ya zao hili katika soko la dunia, wakati gharama za uzalishaji ni kubwa," alisema.

Mtafiti wa Kahawa wa TACRi, Sophia Malinga, akizungumzia baadhi ya changamoto zinazotajwa na wakulima wa kahawa, aliwataka wakulima kuendelea kutumia mbegu bora zilizogunduliwa na taasisi hiyo na kufuata kanuni za kilimo cha kahawa ili kuzalisha kwa wingi kahawa ya daraja la kwanza ambayo ina bei nzuri katika soko la dunia.

Habari Kubwa