Zanzibar yatafakari kutumia bodaboda

10Aug 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Zanzibar yatafakari kutumia bodaboda

BARAZA la Usalama wa Barabarani la Taifa na Bodi ya Usafiri wa Barabarani Zanzibar, limetafakari masuala ya kiusalama barabarani ikiwamo kuanza  matumizi ya usafiri wa pikipiki visiwani.

 Aidha, limeangalia pia mienendo ya  tozo za papo kwa papo barabarani, zinazotumiwa Tanzania Bara

Taasisi hizo  zimekutana kujadili namna ya kuimarisha hali ya usalama wa barabarani, katika kikao kilichofanyika Mjini Zanzibar kikiwa chini ya Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni.

Akizungumza na wanahabari baada ya kumalizika kwa kikao hicho Naibu Waziri Masauni, alisema pia wamejadili kuruhusu sheria ya matumizi ya bodaboda kama nyenzo ya usafirishaji kwa Zanzibar.

Alisema pamoja na mambo mengine, kikao  kilijifunza masuala ya matumizi ya tozo ya papo kwa papo ambayo inatekelezwa Tanzania Bara.

Alieleza kuwa mchakato huo kwa Zanzibar utakapoanza ni vyema kujifunza changamoto zinazojitokeza kwa Tanzania Bara kabla ya  utekelezaji.

Alisema lengo ni kudhibiti mianya ya athari ambayo inaweza kusababishwa na matumizi ya pikipiki.

“Pia tumejadili kuhusu mikakati na malengo tuliyojipangia na kujadiliana ambayo tumeona mambo ya kuyasisitiza ni suala la ukaguzi wa magari ambapo tayari tumeshatoa maelekezo na miongozo kuwa utaratibu wa kutoa stika za magari kiholela ndio mwisho wake na badala yake sasa kila stika inayotolewa ni lazima gari iwe imekaguliwa na kujiridhisha ubora wake”alisema Masauni.

Aidha, alisema kuwa kusitisha kwa sherehe za maadhimisho ya wiki ya usalama wa barabarani kumeleta faida ambapo fedha zilizotarajiwa kutumika katika maadhimisho hayo zinunulie magari kwa kila mkoa ili kupunguza changamoto ya usafiri kwa askari wa barabarani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu, alisema  kuna mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza ajali za barabarani ambapo ajali hizo zimepungua kwa asilimia 22.5 mwaka huu.

Alisema tathmini inaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi mitano kuanzia Marchi hadi Julai mwaka huu kulitokea jumla ya ajali za barabarani 1239, vifo 674 na majeruhi ni 1289.

“Kwa miezi mitano kutoka Machi hadi Julai mwaka jana kulitokea ajali 1,598, vifo 796 na majeruhi ni 1660”alisema kamishna huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usafiri wa Barabarani Zanzibar Muhammed Simba, alisema kuwa wapo katika maandalizi ya kuruhusu usafiri wa bodaboda hivyo ni vyema kujifunza kwa Tanzania bara namna ya kuweza kudhibiti ajali.

“Tumeona ni vizuri kujifunza na hapa tumeoneshwa utaratibu wa kudhibiti bodaboda tokea inapotoka na kujua mwendendo mzima wa watumiaji wa bodaboda hivyo wasiwasi tulionao kutokana na madhara ya usafiri huo utaondoka iwapo mifumo hiyo itatumika vizuri,”alisema Kamishna huyo.

Habari Kubwa