Mwalimu Mkuu asimulia anavyoshika chaki pekee yake kwa wanafunzi 366

10Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwalimu Mkuu asimulia anavyoshika chaki pekee yake kwa wanafunzi 366
  • Akifundisha leo, kesho hoi anabaki kusahihisha
  • Muhimu darasa 4 na 7; wengine wafundishana
  • Aliyekodiwa kwa Sh. 500 hakulipwa, akasusa
  • Ashukuru ‘almanusura’ madarasa kutoka NGO

WANAFUNZI wa shule za msingi katika Halmashauri ya Ushetu, waliopo pembezoni mwa halmashauri hiyo mkoani Shinyanga, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kutembea umbali mrefu kutafuta elimu ambayo ndio mkombozi wa maisha yao baadae.

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mikwa, iliyopo Kata ya Mapamba katika Halmashauri ya Ushetu, Elias Zabron, anayewafundisha wanafunzi 366 pekee, akisahihisha kazi za wanafunzi.

Hao wamekuwa wakitembea zaidi ya umbali kilometa 15 kwenda na kurudi katika shule zilizopo kata jirani, hali inayowakwaza kielimu iwe msingi au sekondari. Imekuwa kawaida wanaishia njiani au kutofanya vyema mitihani yao ya mwisho.

Pia, asilimia kubwa ya wanafunzi wamekuwa wakienda kusoma katika shule za msingi zilizopo Kaulia mkoani Tabora, hali ikiwa mbaya, wasichana wanasusia masomo, wanabaki kulea wadogo zao, kuchunga mifugo na kuwa mama wa nyumbani.

Hivyo, kutokana na adha hiyo, Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP), kwa kushirikiana na Serikali lilianzisha utaratibu wa kujenga vyumba vya madarasa na ofisi katika shule za msingi na sekondari jirani, asilimia kubwa ikitoka katika nguvu za wananchi.

Ni utaratibu uliyoisaidia Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga kutatua changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali, zilizopo pembezoni mwa halmashauri hizo.

Hapo inajumuisha ujenzi wa shule shikizi zinazosaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.

Pia, kuna suala la uanzishaji miradi katika shule za msingi, ikiwamo ufugaji nyuki, ili shule kujiendesha au kutatua baadhi ya changamoto shuleni, pasipo kutegemea serikali.

Ni miradi inayowasaidia wanafunzi kujifunza stadi za ufugaji na baadae wamalizapo elimu zao, wanajikuta na stadi kamili kama za ufugaji na utunzaji mazingira.

Mwalimu Mkuu

Eliasi Zabroni ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Mikwa, iliyopo katika Kata ya Mapamba, katika Halmashauri ya Ushetu. Anasema, shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 366 ikiwa na vyumba vya madarasa vitatu.

Huo ni msukumo mmojawapo uliofanya Equip kuwajengea vyumba viwili vya madarsa na ofisi ya walimu. Anasema, awali kabla ya kujengwa shule hiyo, wanafunzi walitembea umbali wa kilomita 30 kwenda shule 15 na kurudi.

Zabroni anasema wanafunzi wengi shulenu kwake waliotoka kijiji cha Mikwa, wakishindwa kufika shuleni na kulazimika kutembea umbali kilomita 13 katika shule za msingi  katika Halmashauri ya Uyui, Mkoani Tabora, kuepuka safari ya kilomita 30.

Anasema ni hali iliyowafanya wakazi kuanzisha ujenzi wa shule shikizi, huku Equip likiwasaidia umaliziaji.

 

Zabroni anasema, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 366 kuanzia darasa la awali hadi la tatu, vyumba vitatu vya madarasa na mwalimu mmoja.

Ni changamoto inayomkabili Mwalimu Zabroni, akisema, wamefikia hatua baadhi ya wanafunzi wenye uwezo bora darasani, kufanya kazi ya kuwasaidia wenzao wa madarasa ya chini; darasa la awali na la kwanza.

Mwalimu Mkuu anasema, wingi huo wa wanafunzi umemfanya alazimike kufundisha kwa awamu na wakati mwingine anakijikuta anafundisha darasa la tatu muda mrefu na kuwafanya wanafunzi madarasa ya awali, la kwanza na pili kukosa huduma  yake na wanalazimika kufundishwa na wenzao.

Pia, binafsi anakiri kuchoka sana siku moja baada ya kufundisha, anaishia kusahihisha madaftari ya wanafunzi, hali inayodidimiza kiwango cha ufaulu shuleni.

Anasema, inapotokea anaugua kipindi chote wanafunzi hao wanakosa masomo, hivyo anaomba kuongezewa walimu wa kumsaidia.

“Wakati shule inaanzishwa wazazi waliajiri mwalimu ambaye alikuwa anawafundisha wanafunzi hao na kila mzazi mmoja alikuwa akichangia kiasi cha shilingi mia tano, kama moja ya malipo ya kumlipa mwalimu.

”Lakini tangu nimefika, hawajawahi kulimpa mwalimu na kumfanya mwalimu huyo kushindwa kufundisha na kuniachia kila kitu mimi mwenyewe,” analalamika  Mwalimu Zabroni.

Uongozi Halmashauri

Leuvenic Bwire, Kaimu Ofisa Elimu wa Kata ya Mapamba, anatoa historia, shule hiyo ilianza na wanafunzi 100 hadi sasa inakidhi hadhi ya shule kamili, kutokana na msaada wa asasi ya Equip kujenga madarasa.

Pia, anasema kujengwa kwa shule hiyo kumesaidia wanafunzi wengi waliokuwa wameacha masomo wakitembea umbali mrefu

Michael Matomora, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, naye anakiri tatizo la shule ya Mapamba na juhudi za wazazi kujenga madarasa ya shule shikizi.

Anasema kwa sasa shule imesajiliwa kutokana na kukidhi masharti, ikiwa sambamba na shule shikizi tatu katika halmashauri yake, ambazo ni Kawekamwe iliyoko katika kijiji cha Isanga kata ya Inadahina yenye wanafunzi zaidi ya 200 na Shule ya Msingi Mliza, katika Kata ya Bukomela yenye zaidi ya wanafunzi 400.

Kuhusu walimu, Matomoro anasema alitarajiwa kupatiwa walimu mwezi uliopita, ambako wamepatiwa walimu watatu wapya, kumsaidia mwalimu mkuu..

Pia, anatoa rai wa wazazi katika eneo hilo kubadilika, kuachana na mila potofu ya kuwakandamiza wasichana kuwanyima fursa za masomo.

Simon Berege, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, anayesema kuwa, Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP) kufika katika Halmashauri hiyo, umeleta mabadiliko makubwa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na miradi mbalimbali ya elimu, kwani wananchi walijitahidi kujenga vyumba vya madarasa ambavyo ukamilishaji uliishia njiani.

Hadi sasa kuna vyumba vya madarasa 62 wakibakiwa na upungufu wa vyumba 45, katika mahitaji yao shule za msingi.

Aidha, Berege anasema kuwa katika awamu ya kwanza kulikuwapo vyumba vitano, ofisi za walimu tatu na matundu 10 ya vyoo vilivyojengwa katika shule za msingi za Maliasili Kata ya Mwalugulu; Mwamalulu, Kata ya Jana na Madaho katika kata ya Lunguya.

Berege anasema, katika awamu ya pili walijenga na kukamilisha vyumba vya madarasa saba, ofisi za walimu tatu na matundu ya vyoo 12 katika shule za msingi: Nyakadoni B, Umbogo kata ya Mwanase, Nyangaka kata ya Bugarama na Nhumbi kaya ya Mwakata.

Pia, anasema kupitia mradi huo wa Equip, ulianzisha mpango wa Kusoma, Kuandika na Kuelewa(KKK), hali inayosaidia asilimia mkubwa ya wanafunzi, ikipandisha daraja kiwango cha wasioelewa katika halmashauri, kutoka asilimia sita hadi asilimia  mbili.

Berege anasema, waliwapatia pikipiki Waratibu Elimu, ili kuwasaidia kufika maeneo ya changamoto na kuwapa mafunzo ya kuongeza ujuzi katika kuwafundisha wanafunzi.

Maofisa Elimu

Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wa hamalsahuri hiyo, Eliyuko Mbaga, anasema Equip imeanzisha miradi ya ufugaji nyuki, kilimo cha mpunga na mahindi katika shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Msalala.

Anadokeza kuwa, zaidi ya shule za msingi tatu zimenufaika na miradi hiyo, ambazo ni: Ntandu, yenye zaidi ya mizinga ya asali na nyuki 30; Ndala, ina mizinga 40  na shule ya Shishinulu, yenye mizinga 22 na ilivuna lita 34 za asali.

Mbaga anasema mapato hayo yametumiwa kununua chakula cha wanafunzi na kugharamia maandalizi ya mitihani ya kila mwezi kwa ajili ya majaribio ya wanafunzi, hasa wa darasa la nne na saba ambao wanakabiliwa na mitihani ta taifa.

Mbaga anasema, pia imesaidia kupunguza michango kwa wazazi na watoto kupata muda wa kutosha kusoma darasani, ikilinganishwa na walivyokuwa wakienda majumbani kupata mlo wa mchana .

Matrida Tunge, ni Ofisa Elimu  wa Kata ya Malunga, katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, anasema, Shule ya msingi Malunga ilikuwa na vyumba vya madarasa tisa tu, kuwafanya wanafunzi kusoma kwa awamu, lakini kwa hali ni tofauti, baada yua kupatikana vyumba vya madarasa vipya, ufualu umeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2017, hadi asilimia 78, mwaka jana, mwaka  huu wakitarajia kufikia asilimia 95 ya ufaulu.

Habari Kubwa