Zifahamu taratibu za kusajili NGOs

10Aug 2019
John Juma
Nipashe
Zifahamu taratibu za kusajili NGOs

NENO NGOs ni  kifupisho  cha  maneno  Non-Governmental   Organisations  na kwa  Kiswahili humaanisha mashirika au asasi zisizo za kiserikali.

Kama kawaida  serikali  ina  utaratibu wa kumiliki na kusajili mashirika  yake, kwa  mfano  Shirika  la  Bima la Taifa, Shirika  la Nyumba NHC, la umeme-Tanesco na lile la Chakula na Lishe (TFNC) yote haya inayaanzisha na kuyamiliki.

Lakini tunapozungumzia  NGOs  maana  yake ni  kuwa  ni mashirika  ambayo  kwa  namna  yoyote  ile  serikali haihusiki  na  umiliki  wake wala haihusiki na kazi zake mbali na kushirikiana nayo.

 Ni  asasi ambazo  humilikiwa  na   watu  binafsi, wanataaluma na mengine yanamilikiwa na watu wa kimataifa.  Serikali hushirikiana  nayo  tu lakini  si  kuyamiliki.

Taratibu  za  uanzishaji,  usajili  na uendeshaji  huratibiwa bayana  na  sheria  ya  mashirika  yasiyo  ya  kiserikali namba  24, ya mwaka  2002.

MALENGO YA KUANZISHA NGO

Malengo  makuu  ya  kuanzisha  NGO  mara nyingi  ni  kusaidia  makundi  au  kundi  maalum  katika  jamii.  Asasi ya kiraia  sio  shirika  la  biashara. Wala si  kampuni  ambayo  muanzishaji  wake hutarajia  kutengeneza  faida. NGO  ni  shirika  la  hisani na la  kujitolea  kusaidia  makundi  katika jamii.

Ni bayana kuwa usitegemee  kuanzisha  NGO  kwa  ajili  ya  kutengeneza  faida  hasa kupata   fedha.

 USAJILI  WA  NGO.

Usajili  wa  NGO  umegawanyika  katika  makundi  makuu  manne. Kwa  mujibu  wa  sheria  mgawanyo  huu  umelenga  maeneo  ya  kijiografia. Hata  hivyo  ada  za  usajili  na  mambo  mengine  muhimu  katika  usajili   hutegemea  mpangilio na mgawanyo  huu. 

Kwanza  kuna  mgawanyo  wa usajili  wa  ngazi  ya  wilaya, ambao  huiwezesha  NGO  kufanya  shughuli  zake  ndani  ya  mipaka  ya  wilaya inayohusika.  Husajiliwa  hapo hapo  wilayani  na  hufanya  kazi  zake  ndani  ya  mipaka  hiyo na haiwezi kutoka nje.

Aidha, kuna usajili wa pili wa ngazi  ya  mkoa. Huu huhusisha  usajili ngazi  ya   mkoa na  mipaka ya  kazi  itakuwa  ni  ndani  ya  mkoa  husika.

Halikadhalika kuna usajili wa aina ya tatu  huu ni  usajili  ngazi ya  taifa  ambao  hufanyika  makao makuu  na  mipaka  ya  kazi  ni  taifa  zima.

Kuna usajili wa aina ya nne ambao ni   usajili  ngazi  ya  kimataifa  ambao  huiwezesha  NGO kufanya  kazi  zake katika  taifa  zaidi  ya  moja.

OFISI ZA  USAJILI

Kama unahitaji kuwa na NGO ngazi  ya  wilaya  utalazimika kwenda  makao  makuu  ya  wilaya  yako kwa ajili ya kufanyika usajili, hivyo  ulizia  ofisa  maendeleo  ya  jamii.  Hawa  ndiyo  huhusika  na  usajili. Halikadhalika  ngazi  ya  mkoa utakwenda  makao  makuu  ya  mkoa  wako   ndipo  usajili  utakapofanyika.

Aidha  kwa  ngazi  ya  taifa  usajili  hufanyika   kwa  msajili  wa  NGO. Kwa  sasa  wizara  husika  ni  Wizara  ya  Maendeleo  ya  Jamii,Jinsia  na  Watoto. Wasajili  wa  ngazi  zote  hupata  mamlaka  ya  kusajili kutoka  kifungu  cha  22(1) cha  sheria  ya  mashirika  yasiyo  ya  kiserikali.

VITU  MUHIMU

Ili kufanikisha usajili nyaraka muhimu ni pamoja na Katiba  ya NGO.  Hizi  hutakiwa  nakala  tatu  zilizojaladiwa au kufanyiwa ‘ binding.’

Maelezo binafsi ya  viongozi  watatu wa  NGO. Mwenyekiti, Katibu  na  Mhazini.  Maelezo  binafsi  ni  wasifu( CV) pamoja  na  picha  mbili  za  kila  mmoja.

Mukhtasari  wa  kikao  cha  kuanzishwa  kwa  NGO  ukienda  sambamba  na  majina na  sahihi  za  waanzilishi.

Fomu  ya  maombi  ya  usajili  iliyojazwa ( NGO form namba 1). Hii hupatikana  kwa  msajili. Itatakiwa  kubandikwa  ushuru  wa  stempu wa  Shilingi 1,500.

Nyaraka nyingine muhimu ni barua  ya  utambulisho  kutoka kwa  ofisa  maendeleo  ya  jamii  wa wilaya au  mkoa  husika.

Aidha jiandae na kuwasilisha taarifa  nyingine  yoyote  ambayo  msajili  anaweza  kuomba kutoka  kwako.

ADA  ZA  USAJILI

Kwa ngazi  ya  wilaya  ni Shilingi 80,000,  mkoa ni 100,00 na kwa ngazi  ya  taifa ni Shilingi  115,000  na  kimataifa  ni Dola  za  Kimarekani 350.

Habari Kubwa