Serikali iziongezee uwezo shule za Kata kitaaluma

10Aug 2019
Reubeni Lumbagala
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali iziongezee uwezo shule za Kata kitaaluma

SERIKALI inamiliki shule mbalimbali za msingi na sekondari, zikiwamo za kata.

Baadhi ya shule za kata zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, hali inayosababisha baadhi ya watu kuzidharau na kuzibeza kwa kudhani changamoto hizo haziwezi kuleta matokeo chanya katika mitihani ya Taifa.

Mtazamo huu unapaswa kubadilika sasa kwani matokeo ya mitihani ya kidato cha Sita mwaka huu, yamedhihirisha pasi na shaka juu ya uwezo mkubwa walionao wanafunzi wasomao katika shule hizi kutokana na kufanya vizuri katika mitihani hiyo.

Katika Matokeo ya mwaka huu yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yanaonyesha ufaulu umepanda kutoka asilimia 97.58 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 98.32 mwaka huu  ikiwa ni sawa ongezeko la asilimia 0.74 ya ufaulu.

Habari njema katika matokeo hayo ni kuwa, katika shule kumi bora kitaifa, zipo shule mbili za Kata (Shule ya Sekondari Kisimiri na Muriet) za mkoani Arusha na katika shule 100 bora, zipo shule 52 za kata.

Juhudi kubwa zilizofanyika kufanikisha mafanikio haya ya shule za Kata katika matokeo ya kidato cha Sita, zinapaswa kuendelezwa ili kustawisha mafanikio zaidi.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwenye shule mbalimbali za sekondari za Kata, upo umuhimu mkubwa wa serikali kuziongezea uwezo shule hizi ili ziendelee kutoa matokeo bora.

Shule ya Sekondari Kisimiri ambayo imeshika nafasi ya kwanza katika matokeo haya, ina changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Kutokana na changamoto hii, uongozi wa shule kwa kushirikiana na wazazi na walezi, wameajiri walimu sita wa muda ili kutatua changamoto hiyo.

Naungana na uongozi wa shule na wazazi ambao wameridhia kuchangia fedha kwa ajili ya kuajiri walimu hao ili watoto wao waweze kupata elimu bora.

Hata hivyo, naishauri serikali kupeleka walimu wa ajira mpya sita kwa masomo ya sayansi katika shule hiyo ili kutatua changamoto hiyo.

Njia mojawapo ambayo serikali inapaswa kufanya ili kuiunga mkono shule hiyo kutokana na mafanikio iliyoyapata katika mitihani ya Taifa, ni pamoja na kuajiri walimu wapya wa kwenda kuukabili upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Walimu wa ajira za kudumu watakuwa na muda wa kutosha kuwasaidia wanafunzi hata kupitia muda wa ziada kuliko walimu wa muda.

Kisimiri ni mfano tu wa shule nyingi za kata zenye upungufu wa walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia, Baolojia na Hisabati.

Kutokana na umuhimu wa masomo ya sayansi katika kuchagiza maendeleo ya viwanda, serikali iajiri walimu wa kutosha kwenda kufundisha shule za kata kwa maendeleo ya taaluma.

MABWENI

Changamoto nyingine ni ukosefu wa mabweni katika shule nyingi za kata. Mabweni ni nyenzo muhimu ya kusaidia wanafunzi kupata muda wa kutosha kujisomea kutokana na kushindwa kusoma ipasavyo wanapokuwa katika mfumo wa kutwa.

Hivyo basi, kupitia ujenzi wa mabweni katika shule za Kata, ukuaji wa taaluma utaongezeka maradufu. Muhimu ni wadau wa elimu, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla, kushiriki kikamilifu katika kuchangia ujenzi wa mabweni.

NYUMBA ZA WALIMU

Ukosefu wa nyumba za walimu ni changamoto nyingine kubwa katika shule za kata. Walimu wakikaa karibu na shule watakuwa na muda mwingi wa kuwafundisha wanafunzi wao na kuchangia katika ufaulu.

Ujenzi wa nyumba za walimu unapaswa kutiliwa mkazo mkubwa na serikali kwa shule za kata ili kuleta ustawi wa taaluma.

Serikali pia izijengee uwezo shule za kata, ili shule hizo ziweze kupata vitabu vya kiada na ziada kwa minajaili ya kuchochea ufundishaji na ujifunzaji wenye tija shuleni.

Aidha, changamoto za madawati, maabara, vifaa vya maabara, vyumba za madarasa, vyoo, mifumo ya maji, zinapaswa kutatuliwa ili mazingira ya ujifunzaji yawe bora.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amezipongeza shule za Kata kwa kufanya vizuri katika matokeo ya Kidato cha Sita.

Jafo anasema: “Haya ni mapinduzi makubwa, wengine walikuwa wakizibeza hizi shule, na huu ni ujumbe kwamba kwa wazazi ambao matokeo ya kidato cha nne yakitoka wanakimbilia shule zenye jina maarufu sasa waacheni watoto huko kwenye shule za kata, watulie wasome.”

Wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na shule za kata wajiamini na wasome kwa bidii kwani wana uwezo wa kufanya mapinduzi makubwa ya kitaaluma.

Juhudi zilizofanywa na serikali za kukarabati shule kongwe, zifanyike pia katika shule za msingi na za sekondari za kata ili kuwavutia wazazi na walezi kuruhusu watoto wao kusoma katika shule hizo na hatimaye kukuza taaluma na ufaulu.