Hatima Lissu Ubelgiji kujulikana Agosti 20

10Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Hatima Lissu Ubelgiji kujulikana Agosti 20

MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anatarajiwa kupimwa kwa mara ya mwisho na madaktari wake na kupewa ruhusa ya kutoka hospitalini Agosti 20.

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Lissu ambaye ni mtaalamu wa sheria yuko Ubelgiji akiendelea na matibabu ya kibingwa yaliyoanzia Tanzania Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi alipofika nyumbani kwake akitokea bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha juzi, kaka wa Lissu, Wakili Alute Mughway, alisema familia yao inamshukuru Mungu kwa kumwona ndugu yao na kuonyesha ukuu wake.

Alisema kwa sasa, wanajiandaa na ujio wa Lissu Septemba 7, mwaka huu kama hatakuwa na mabadiliko ya ratiba ya kurejea kwake Tanzania.

Wakili Alute alisema kuwa baada ya Lissu kutua nchini, watakwenda mahakamani kudai haki yake ya kutolipiwa gharama za matibabu nje ya nchi pamoja na posho zake za ubunge.

Alisema kuwa Lissu pia atafuatilia kwenye vyombo vya ulinzi kujua walikofikia juu ya uchunguzi wa tukio lake la kusudio la kumuua na kuwafahamu waliohusika kufanya tukio hilo la kinyama.

Alisema Lissu pia ataungana na mawikili wanne aliowaweka kupinga mahakamani kuvuliwa kwake ubunge na tayari hatua za kwanza za kesi yake imeshafunguliwa Agosti 2, mwaka huu na kupewa jalada la maombi namba 18/2019.

Alisema yeye ndiye amepewa nyaraka zote zilizowasilishwa mahakamani na ndiye mwenye madaraka ya kisheria kutia saini kwa niaba ya Lissu.

Sambamba na hilo, Alute alisema Lissu ataiomba mahakama kuzuia ubunge wa mbunge mteule wa Jimbo la Singida Mashariki kwa madai kuwa hatua za kumpata mrithi wake huyo zimefanywa kwa "roho mbaya".

"Spika (Job Ndugai) alitangaza bungeni amemvua ubunge kwa roho mbaya na alikusudia kufanya hivyo kwa sababu dalili zilionekana za kumnyima mshahara wake kwa miezi mitatu baada ya kelele akamrudishia," alisema.

Alisema maombi ya Lissu mahakamani yatasimamiwa na jopo la mawakili wanne ambao ni Peter Kibatala, Jeremiah Mpobeswa, John Mallya na Fredy Kalonga.

Alute alisema wameamua kuweka idadi hiyo ya mawakili kwa sababu kisheria maombi hayo yanaweza kuonekana ni rahisi, lakini yakawa na uzio wa kisasa.

Habari Kubwa