Waziri akuta wachimbaji madini wanajisaidia mtoni

10Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
GEITA
Nipashe
Waziri akuta wachimbaji madini wanajisaidia mtoni

NAIBU Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima, amewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kata ya Mgusu mkoani Geita kufuata taratibu za hifadhi ya mazingira ili kunusuru afya zao na kuchukua tahadhari ya kukabiliana na uwezekano wa milipuko ya magonjwa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima

Alitoa tahadhari hiyo jana baada ya kufanya ziara ya kikazi kutembelea eneo hilo kuona uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.

Akiwa katika eneo, Sima alisema bado kuna tatizo la uchafuzi wa mazingira katika maeneo wanayoyatumika kuchenjua dhahabu kwa kutumia zebaki, na kuna haja wachimbaji hao kukaa na Halmashauri ya Geita Vijijini ili kuhakikisha wanakuwa na vyoo bora.

Naibu waziri huyo pia alitoa kauli ya serikali kuhusu mpango kazi wa taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika shughuli za uchenjuaji, akiwataka wakazi wa Mgusu kuendelea na shughuli za uzalishaji wa dhahabu bila kuathiri mazingira kwa kupunguza matumizi ya kemikali hiyo inayoharibu mazingira na afya za binadamu.

“Nimeona namna vijana wanavyojishughulisha kwa ajili ya kujipatia kipato, hili ni jambo jema kwa taifa letu, lakini nimetembea hadi chini kwenye ule Mto wa Nyamasenge, hakuna vyoo, watu wanatumia pori na mto kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.

“Kwa mazingira yetu ni hatari sana, tunaweza kufanya kazi nzuri lakini ugonjwa utasitisha shughuli zetu. Nawasisitiza kuwa usafi ni jambo la kwanza katika kufanya kazi, huwezi kuwa na nguvu isiyojali usafi,” Sima alisema.

Katika ziara yake hiyo, naibu waziri huyo pia alitembelea chanzo cha maji cha Mto Mabubi na kujionea hali mbaya inayotishia kutoweka kwa chanzo hicho kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea kandokando ya eneo hilo.

“Chanzo cha maji cha Mto Mabubi hakitadumu na maji hayatakuwa salama kwa matumizi ya binadamu endapo kitaendelea kuingia kemikali ya zebaki, nanyi wachimbaji kujisaidia katika eneo hilo," Sima

alionya.

Diwani wa Kata ya Mgusu, Pastory Ruhusa, alisema ataitisha mkutano wa wananchi mapema iwezekanavyo ili kuweka mikakati ya haraka kutokomeza hali hiyo.

Sima yuko katika ziara ya kikazi Kanda ya Ziwa kukagua uzingatiaji na usimamizi wa Sheria ya Mazingira na uelimishaji wananchi kuhusu mpango wa serikali wa kupunguza matumizi ya zebaki nchini.