Lukuvi atoa siku 30 za uchunguzi maofisa 183

10Aug 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Lukuvi atoa siku 30 za uchunguzi maofisa 183

SERIKALI imetoa siku 30 kukamilika kwa uchunguzi dhidi ya maofisa 183 wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi waliosimamishwa kazi juzi.

William Lukuvi

Maofisa hao walisimamishwa na Waziri wa Wizara hiyo, William Lukuvi kwa tuhuma mbalimbali za rushwa na kuikosesha serikali mapato kwenye sekta ya ardhi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri Lukuvi alisema ameunda timu kwa ajili ya uchunguzi wa watendaji waliohujumu mfumo wa ulipaji malipo ya viwanja.

Alisema timu hiyo itawajumuisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), pamoja na taasisi nyingine ambazo zina wataalamu wanaohusika na mifumo inayotumia mitandao.

Alisema uchunguzi wa timu hiyo utafanyika kuanzia miaka mitatu iliyopita yaani 2016 hadi 2019, ambapo mfumo huo wa kulipia viwanja ulianza kutumika.

Hata hivyo, Lukuvi alisema watendaji waliosimamishwa kazi wamebainika kwamba walifanya ujanja huo ndani ya miezi sita ya mwaka wa fedha 2018/19 ambapo mfumo wa malipo Hazina ambao umeonyesha moja kwa moja.

"Naomba muelewe hawa waliosimamishwa hivi sasa ni wale walioiibia serikali kuanzia Sh. 100,000 na kuendelea lakini katika uchunguzi utakaofanywa hata kama umeiibia serikali Sh. moja utachukuliwa hatua za kisheria," alisema Lukuvi.

Alisema lengo la kutoa siku hizo chache za uchunguzi ni kutokana na mfumo kuonyesha kila kitu hivyo hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kufanya uchunguzi.

"Nimesikia malalamiko kwamba waliosimamishwa wanasema watu wamewaibia (Password zao), si kweli hayo ni mawazo yao walijisahau kwamba mfumo wa malipo wa Hazina unaonyesha moja kwa moja ndicho kilichowakamatisha wasidanganye watu," alisema Lukuvi.

Alisema waliobaki wajiandae na zoezi hilo maana baada ya uchunguzi kuna majina mengine yatabainika kwa sababu wanaanzia kuchunguza tangu mfumo ulipoanza kutumika.

Hata hivyo, Lukuvi alisema tayari amewabaini watu ambao wameshiriki kufutiwa madeni na wamekaa kimya bila kutoa taarifa na kwamba nao watatakiwa kulipa gharama ambazo wameidhulumu Serikali.

Alitoa mfano wa kiwanja kilichopo mkoani Mbeya ambacho kilikuwa na mita za mraba 20,234 lakini katika mfumo amejaziwa mita za mraba 502, ambapo amekuwa akilipa Sh. 63,000 kwa mwaka badala ya Sh. milioni sita kwa mwaka.

Alisema utapeli huo umeisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 68 tangu wakati huo hadi hivi sasa.

"Naomba nimwambie mwenye kiwanja hicho kama anajua jina hilo ajiandae kulipa fedha hizo pamoja na faini kwa sababu ameiibia Serikali pamoja na kuchelewa kulipa ndani ya muda husika," alisema Lukuvi.

Alisema kwa walioshirikiana na watendaji wa Wizara hiyo kufanya mchezo huo wasifikiri wako salama kwani watalipa kiasi cha fedha ambacho amefutiwa deni ikiwamo kupunguziwa ukubwa wa kiwanja ambacho amekuwa akilipa fedha pungufu.