TBS yawaita wanaotaka kufanya biashara SADC

10Aug 2019
Joseph Mwendapole
DAR ES SALAAM
Nipashe
TBS yawaita wanaotaka kufanya biashara SADC

WAFANYABIASHARA nchini wanaotaka kufanyabiashara zao kwenye nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamehimizwa kwenda ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili wapatiwe elimu kuhusu namna ya kufanya biashara na nchi hizo bila vikwazo.

Ushauri huo ulitolewa jijini Dar es Salaam jana na Ofisa Mwandamizi wa Uhakiki Ubora wa TBS, Stella Mrosso, wakati akizungumza kwenye Maonesho ya Nane ya Wiki ya Viwanda SADC yaliyomalizika jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumzia faida za wafanyabiashara kupata elimu TBS kabla ya kupeleka biashara zao kwenye soko la nchi za SADC, Mrosso alisema hatua hiyo itawasaidia kujua taratibu za kufuata ambazo zitawasaidia kuepukana na vikwazo mbalimbali.ā€¯Utaratibu huu utarahisisha biashara kuliko wale wanaopita juu kwa juu, kwa sababu wanaweza kufika mipakani wakazuiwa kupeleka bidhaa zao kwenye nchi walizokusudia na hivyo kujikuta wakipata hasara kubwa," alisema.

Alisema TBS ni mdau mkubwa kwenye nchi za SADC hasa katika suala zima la umahiri, hivyo wananchi wanapaswa kulitumia shirika hilo ili wasipate shida.

Pia, aliwataka wafabiashara kufika kwenye ofisi za shirika hilo kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kwasababu shirika hilo lina maabara zenye umahiri uliothibitishwa kimataifa.

Alifafanua bidhaa ikishapimwa kwenye maabara zenye umahiri haiwezi kupimwa tena kwa kuwa matokeo yake yanakuwa yanaaminika.Alitaja baadhi ya maabara za shirika hilo zenye umahiri kuwa ni maabara ya nguo, maabara ya kemia, maabara ya ujenzi na maabara ya umeme.

Mrosso alitaja hatua nyingine ambazo zinachukuliwa na nchi za SADC kuondoa vikwazo vya kibiashara kwa nchi wanachama ni kuoanishwa viwango baina ya nchi wanachama.Alisema kwenye nchi za SADC viwango ambavyo tayari vimeoanishwa vinafanyakazi kulingana na mahitaji ya wafanyabiashara wa Tanzania.

Habari Kubwa