Waziri azibana kampuni makato ya upigaji simu

10Aug 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri azibana kampuni makato ya upigaji simu

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuzichukulia hatua za kisheria kampuni za simu zinazowakata wateja wake zaidi ya Sh. 10.40 kwa dakika kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye

Alisema mbali na kuchukuliwa hatua za kisheria, pia zirudishe gharama zote zilizowakata watumiaji nje ya mwongozo wa mawasiliano uliozinduliwa mwaka jana, ukielekeza kampuni za simu kutoza Sh. 10.40 badala ya Sh. 15.60 kwa dakika moja.

Nditiye alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kikazi ya Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji wa  Zanzibar, Sira Ubwa, aliyetembelea TCRA kwa lengo la kujifunza namna mamlaka hiyo inavyofanya kazi.

Alisema kumekuwapo na tabia ya kampuni za simu kutofuata mwongozo huo na badala yake kutoza Sh. moja kwa sekunde (Sh. 60 kwa dakika moja) kinyume cha sheria za mamlaka hiyo.

“TCRA ianze kufuatilia hizi kampuni ambazo zinatoza fedha kinyume cha mwongozo wa mawasiliano, kwanza wawachukulie hatua za kisheria, pia wawatoze faini na kuhakikisha wanarudisha fedha zote walizotoza wananchi kunyume cha taratibu,” Nditiye aliagiza.

Alisema mpango wa serikali ni kuona kufikia mwaka 2020 gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine zinakuwa ni Sh. mbili kwa dakika.

Aliwataka Watanzania kuendelea kujisajili kwa utaratibu mpya kwa ajili ya usalama wao na kuepuka usumbufu wa kumiliki laini nyingi za simu.

“Ikifika muda ambao Rais John Magufuli alipanga kuongeza hadi mwisho wa mwaka huu, ukiisha tutazima laini zote ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, lengo ni kumtambua kila anayepiga simu,” Nditiye alisema.

Habari Kubwa