Simba, Yanga, Azam, KMC  biashara ni asubuhi Caf

10Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga, Azam, KMC  biashara ni asubuhi Caf

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, Simba, Yanga, Azam na KMC leo na kesho watashuka katika viwanja tofauti barani Afrika kuanza kuipeperusha bendera ya nchi katika kinyang'anyiro hicho cha kimataifa.

Katika michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika, Simba na Yanga zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa, wakati Azam na KMC zikibeba jukumu hilo kwa upande wa Kombe la Shirikisho.

Yanga ambayo ilijichimbia visiwani Zanzibar kujiandaa na michuano hiyo, ndiyo timu pekee kati ya wawakilishi wa Tanzania Bara inayoanzia nyumbani ikitarajia kushuka Uwanja wa Taifa leo kuikaribisha Township Rollers ya Botswana.

Simba yenyewe itaanzia ugenini Msumbiji dhidi ya UD Songo na tayari iliondoka jana asubuhi na kuwasili mjini Beira nchini humo mchana tayari kwa mechi hiyo ya raundi ya awali itakayopigwa leo pia.Azam FC nayo iliwahi mapema nchini Ethiopia tangu Jumatano ili kuzoea hali ya hewa ya huko kabla ya kuivaa Fasil Ketema (Ethiopia 1) katika mechi itakayopigwa kesho mjini Gondar kaskazini mwa Ethiopia yalipo makazi ya klabu hiyo.

KMC pia imeshawasili salama nchini Rwanda tayari kwa mechi yao dhidi ya AS Kigali itakayopigwa leo.Hakika si mechi rahisi kwa wawakilishi hao wa Tanzania Bara hasa ikizingatiwa michuano ya msimu huu imeanza mapema kabla ya Ligi Kuu kuanza, jambo ambalo limetoa changamoto kubwa kwa makocha kuweza kuunganisha vikosi vyao kutokana na kuwapo kwa wachezaji wapya.

Lakini pia tunatambua baadhi ya timu hususan Azam FC na KMC, kazi imekuwa ngumu zaidi kutokana na kuwapo kwa makocha wapya msimu huu tofauti na Simba na Yanga ambazo zinaendelea kunolewa na Mbelgiji Patrick Aussems na Mwinyi Zahera raia wa DR Congo waliozinoa msimu uliomalizika. Lakini bado, klabu hizo kongwe nchini, kwa makocha hao wamekabiliwa na changamoto ya kuwaunganisha wachezaji wao kutokana na kusheheni nyota wengi wapya.

Hata hivyo, hilo halitutii hofu sana kwani tunaamini kwa maandalizi yaliyofanywa na timu zote, yanatupa imani ya wawakilishi hao kuweza kuipeperusha vema bendera ya nchi kwenye michuano hiyo ya kimataifa na hatimaye kutetea nafasi hiyo ya Tanzania kuendelea kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, Caf.

Tunatambua hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo, na fursa hiyo imejitokeza kutokana na Simba msimu uliopita kufanya vizuri na hivyo Tanzania kuvuna pointi nyingi zaidi ya mpinzani wetu wa karibu Kenya aliyekuwa akiwania nafasi hiyo kwa kutegemea Klabu ya Gor Mahia  kufika mbali zaidi kwenye Kombe la Shirikisho, lakini mambo yakaenda ndivyo sivyo.

Hivyo, kinachowezekana kwa Tanzania kuendelea kuingiza timu nne, ni kwa klabu zote kupigana kufa au kupona ili angalau kufika hatua ya makundi na kisha robo fainali ya michuano hiyo kwani huko ndipo pointi huanza kutolewa kwa nchi kulingana na mafanikio ya klabu zinazoiwakilisha.

Kwa maandalizi timu zote zilizoyafanya kwa Simba kuweka kambi Afrika Kusini na kushinda mechi zake za kirafiki bila kupoteza kabla ya kurejea na kushinda 3-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwenye mchezo wa kirafiki kama ilivyo kwa Yanga ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kariobangi Sharks na kisha kwenda kujichimbia Zanzibar na kujipima nguvu na Mlandege na Malindi, huku Azam nayo ikiichapa TP Mazembe Kagame Cup na KMC ikiichapa Kariobangi Shakrs 2-1, ni ishara ya maandalizi mazuri. Nipashe tunaamini ushindi utapatikakana leo na kesho kwa wawakilishi wetu hao.