Simba wakifuata ya Kilomoni itarudi kuwa ya Ligi Kuu tu

10Aug 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba wakifuata ya Kilomoni itarudi kuwa ya Ligi Kuu tu

KUMEKUWA na msuguano kwa muda wa wiki mbili sasa kati ya aliyekuwa mdhamini wa klabu ya Simba, Hamisi Kilomoni na uongozi wa klabu hiyo.

Ilifika wakati mzee huyo alikamatwa kwa muda na Jeshi la Polisi kwa madai ya kufanya mkutano nyumbani kwake bila kibali. Aliachiwa baadaye, lakini akaambiwa iwapo anataka kufanya mkutano basi akaombe kibali.

Hata hivyo, alifanya mkutano wake siku chache baadaye. Mzee Hamisi Kilomoni anaweza kuwa na hoja, lakini anavyotaka kuwasilisha ndipo anapoleta mkanganyiko pamoja na taharuki.

Kwanza kabisa anaonekana kama vile yeye ndiyo Simba zaidi kuliko wenzake wote. Kwa Kilomoni kwa sababu yeye amecheza Simba na kuwa kiongozi, basi wote waliokuja baada ya hapo hawana uhalali zaidi yake.

Inawezekana kabisa Kilomoni akawa hayuko peke yake kwenye hili. Nyuma ya pazia kunaweza kuwa na wanachama wengine wa klabu ya Simba ambao wanapinga mabadiliko ya uwekezaji.

Walio nyuma ya Kilomoni inawezekana kuwa ni wanachama maarufu na wazito wa klabu hiyo na wengine wameshawahi kuongoza, lakini wanaona aibu kujitokeza kwa sababu hakuna atakayewaelewa wakipinga masuala ya uwekezaji kwenye klabu za soka.

Kuna watu wamenufaika sana na klabu hizi na hata wamepata vyeo, ubunge, nyumba na hata kujimudu kimaisha kupitia klabu hizi.

Watu kama hawa hawawezi kufurahia mfumo huu kwa sababu unakuwa na uwazi zaidi kwenye masuala ya pesa na uendeshaji, tofauti ya ule wa zamani ambao Mwenyekiti wa Klabu na Makamu wake ndiyo wanakuwa watendaji wakuu.

Kwa miaka zaidi ya 80, Simba na Yanga zimekuwa zikiendeshwa kwa mfumo huo wa wanachama ambao wanachagua Mwenyekiti na Makamu, Katibu na Kamati ya Utendaji, lakini hadi leo hii hazina hata viwanja vya mazoezi.

Kwenye klabu hizi kuna viongozi ambao walikuwa wanafaidika kwenye kipindi cha usajili wakipita huku na huko kwa wadau na wafadhili kuomba pesa, lakini wakishapata wanasajili wachezaji wa kiwango cha chini kwa pesa ndogo, zilizobaki zinakuwa za kwao, pia hata mauzo ya jezi.

Hali hii imezidhoofisha sana klabu hizi, badala ya kwenda mbele zimekuwa zikishuka kisoka kwa migogoro isiyokuwa na kichwa wala miguu.

Kuingia kwa wawekezaji kumekuwa ni kama tija kwa soka la Tanzania, kwani baada ya Mohamed "Mo" Dewji kuwekeza Simba kwa mwaka mmoja tu, tayari klabu hiyo imefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Ni kama tulichelewa. Wawekezaji hawa wangekuwa wameingia miaka 10 iliyopita, inawezekana kabisa klabu moja ya Tanzania ingekuwa imechukuwa ubingwa wa Afrika kama Rais Dk. John Pombe Magufuli anavyotamani kuona hilo likitokea kwa sasa.

Tusidanganyane, kila kitu na zama zake. Enzi la soka la ridhaa limekwisha. Wawekezaji hawaepukiki kwa soka la kisasa. Madai ya Kilomoni yanaweza kuwa ya msingi lakini yasisababishe kukimbiza wawekezaji hawa na kama ndio lengo lake, basi enzi hizo zimepitwa na wakati.

Hata wale walio nyuma ya mzee huyo wakae wakijua kuwa kwa sasa hawawezi kuendesha soka la vile ilivyokuwa huko nyuma, kwani imefika wakati mchezaji mmoja anaweza kusajiliwa kwa Sh, bilioni mbili. Bila mwekezaji inawezekana?

Habari Kubwa