Mbunge agharamia taa za uwanja Z'bar

10Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Mbunge agharamia taa za uwanja Z'bar

MWAKILISHI na Mbunge wa Jimbo la Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, Simai Mohammed Said, ameandika historia katika soka la Zanzibar baada ya kuamua kugharamia uwekaji wa taa katika uwanja wa michezo wa Kijiji cha Bungi jimboni humo.

Mbunge wa Jimbo la Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, Simai Mohammed Said.

Akizungumza katika uzinduzi wa taa hizo juzi usiku, Said alisema mchakato huo umewezekana kutokana na kushirikiana na Mbunge Khalifa Salum Suleiman, na wametumia jumla ya Sh. milioni 21.5.

Alisema lengo la mpango huo ni kuwezesha Uwanja wa Bungi kutumika wakati wa usiku kwa michezo mbalimbali hasa ligi za mpira wa miguu na michezo mingine.

Alisema hatua hiyo itachochea vijana kupenda na kushiriki zaidi katika michezo ambayo ni miongoni mwa mambo yanayosisitizwa na ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ikiwa pia sehemu ya ajira.

Naye Mbunge Khalifa Salum alisema  mbali na michezo, hatua hiyo itawapa wananchi fursa ya kuutumia uwanja kwa shughuli za kijamii ikiwamo sherehe za sikukuu, na burudani ambazo kwa kawaida hufanyika hadi usiku pamoja na matukio ya kiserikali.