Yanga, Township Rollers zatishana

10Aug 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga, Township Rollers zatishana

KUELEKEA mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya mwenyeji, Yanga na Township Rollers leo katika Uwanja wa Taifa, miamba hiyo kila mmoja umejigamba kuibuka na ushindi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, alisema wametumia muda wa wiki nne kujiandaa na mchezo huo, na jana asubuhi walifanya maandalizi yao ya mwisho, hivyo ushindi kwao ni muhimu leo.

"Tumejiandaa muda wa wiki nne kwa ajili ya mchezo huu, mapungufu machache tuliyoyabaini kwenye safu ya ushambuliaji tayari tumeyafanyia kazi, naamini hayajirudii tena,"alisema.

Kwa upande wa kocha wa Township Rollers, Tomas Trucha, alisema wamejipanga vizuri kuelekea katika mchezo huo na kufafanua kuwa timu zote zinauwezo mkubwa.

Nahodha wa Township Rollers, Maano Ditshupo, yeye aliahidi kushinda mchezo huo. "Tumejipanga vizuri kukutana na Yanga japo baadhi ya wachezaji waliopo katika kikosi hiki ni wapya sio wale waliokutana na sisi mwaka jana."