Kigogo uchunguzi Takukuru kortini kesi isiyo na dhamana

10Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kigogo uchunguzi Takukuru kortini kesi isiyo na dhamana

MCHUNGUZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyika (44), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyika, akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi. PICHA: MIRAJI MSALA

Mashitaka hayo yanahusisha  kushawishi rushwa ya zaidi ya Sh. milioni 300, kupokea na kutakatisha Dola za Marekani 20,000.

Bosi huyo aliyesimamia uchunguzi wa makosa ya rushwa nchini, alisomewa mashtaka yake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Kevini Mhina.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Paul Kadushi na Simon Wankyo, ulimsomea mshtakiwa mashtaka yake.

Kadushi alidai kuwa katika shtaka la kwanza, Februari 9, mwaka huu eneo la Upanga, mshtakiwa akiwa mwajiriwa na Takukuru kama Mchunguzi Mkuu, aliomba rushwa ya Sh. milioni 200 kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham kwa lengo la kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi tuhuma zilizokuwa chini ya uchunguzi wa mwajiri wake.

Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Februari 10, mwaka huu katika Viwanja vya Maonyesho ya Biashara, Sabasaba vilivyopo Temeke Jijini Dar es Salaam, alijipatia Dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Faizal Hasham kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi dhidi ya Hussein Gulamal Hasham zilizokuwa zinafanyiwa uchunguzi na Takukuru.

Kadushi aliendelea kudai katika shtaka la tatu  kuwa Februari 13, mwaka huu katika ofisi za Makao Makuu ya Takukuru, mshtakiwa akiwa mwajiriwa na Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, alishawishi rushwa ya Dola za Marekani 50,000 kutoka kwa Thangavelu Nallavan Vall kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma zilizokuwa zinamkabili za kukwepa kodi.

Katika shtaka la nne, Wankyo alidai kuwa Februari 14, mwaka huu mtaa wa Haile Selasie karibu na Merry Brown, Wilaya ya Kinondoni alishawishi rushwa ya Dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Nallavan Vall kama kishawishi cha kuharibu ushahidi uliokuwa chini ya uchunguzi wake dhidi ya kukwepa kodi.

Wankyo aliendelea kudai kwamba shtaka la tano, Februari 10, mwaka huu eneo la Sabasaba, mshtakiwa akiwa mwajiriwa kama Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, alipokea Dola za Marekani 20,000 wakati akijua ni zao la kutakatisha na zimetokana na rushwa.

Katika shtaka la sita, ilidaiwa kuwa Februari 19,mwaka huu eneo la Village Super Market katika duka la kubadilishia fedha za kigeni la Electron, mshtakiwa alibadilisha sehemu ya Dola za Marekani 7,000 (alipata Sh. Milioni 16.1)kati ya 20,000, huku akijua ni zao la rushwa.

Katika shtaka la saba, ilidaiwa  Februari 19, mwaka huu eneo la Chamazi Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alinunua ardhi eneo ambalo halijapimwa lenye thamani ya Sh. milioni 15.8, huku akijua fedha hizo ni za kutakatisha na ni zao la rushwa.

Kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu Uchumi, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote.

Hata hivyo, mshtakiwa aliomba Mahakama impe dhamana kwa sababu ana watoto wadogo wanamtegemea.

“Mheshimiwa Hakimu, naomba dhamana nina watoto wadogo hawana mama wa kuwaangalia, wananitegemea mimi,” alidai mshtakiwa.

Hakimu Mhina alisema kesi inayomkabili inasikilizwa Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi, hivyo, mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza na kufanya maamuzi ya maombi yoyote.

"Maombi ya dhamana yanasikilizwa na Mahakama Kuu inayoshughulika na kusiliza kesi yako, utakwenda mahabusu mpaka Agosti 23, mwaka huu kesi yako itakapotajwa tena,” alisema Hakimu Mhina.

Habari Kubwa