Hifadhi ya Mkomazi yaanzisha tuzo maalum

12Aug 2019
Godfrey Mushi
SAME
Nipashe
Hifadhi ya Mkomazi yaanzisha tuzo maalum

HIFADHI ya Taifa ya Mkomazi, imeanzisha tuzo maalum ya jamii na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutambua, kuthamini na kuchochea masuala ya ulinzi wa ikolojia kuzunguka maeneo ya hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Mkomazi

Mpango huo wa Mkomazi kuanza kutoa tuzo hiyo kuanzia mwaka huu, uliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule.

“Nimefurahishwa sana na namna Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilivyojiwekea mkakati maalum wa kulinda ikolojia katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo, hasa baada ya mimi kuitwa kukabidhi tuzo hiyo kwa washindi watano wa vikundi pamoja na shule tano zilizofanya vizuri. Wameanza vyema kwa kutoa fedha kati ya Sh. 200,000 hadi  Sh. 700, 000.

“Wamenieleza  wameanzisha tuzo hiyo kwa jamii na taasisi mbalimbali zinazozunguka hifadhi hiyo ili kuisukuma jamii kujali na kutunza ikolojia ya hifadhi kuanzia mwaka 2019. Ni vizuri na wengine wakaiga mfano huo.”

 Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Abel Mtui, alisema tuzo hiyo inalenga kuongeza mwamko wa jamii kulinda rasilimali za nchi zilizopo katika hifadhi hiyo.

Kamishna huyo ameahidi tuzo hiyo itakuwa endelevu kila mwaka, huku akiiasa jamii kuona umuhimu wa kuitunza na kuilinda Hifadhi ya Mkomazi kama rasilimali ya kujivunia kwa Wilaya ya Same.

Alisema mpango hifadhi hiyo wa kuwatumia faru kama kivutio pekee cha utalii kitakachoitambulisha tofauti na hifadhi nyingine nchini, utaifanya Mkomazi kuwa hifadhi pekee Tanzania yenye kivutio hicho.

Mkomazi hutumika kama kituo kwa ndege ambao husafiri kati ya Bara Ulaya na Afrika. Ni hifadhi inayowavutia wageni wa kimataifa wanaopenda kuangalia aina mbalimbali za ndege.

Ndege hao wanaohama hutumia maeneo ya hifadhi kama vituo vyao vya kupumzikia wakiwa wanaelekea Kusini mwa Afrika au kipindi wanapokuwa wanarudi makwao katika Bara la Ulaya.

Lakini pia, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi imesheheni wanyama kama swala, twiga, cholawa, simba, faru, tembo, pundamilia na mbwa mwitu ambao hutembea kwa makundi na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilianzishwa mwaka 2007 na inapakana na Pori la Akiba la Wanyamapori la Umba lililopo mkoa wa Tanga.

Habari Kubwa