Utajiri wa madini Mwanga watajwa changamoto kubwa

12Aug 2019
Godfrey Mushi
MWANGA
Nipashe
Utajiri wa madini Mwanga watajwa changamoto kubwa

UTAJIRI wa madini ya shaba na jasi (Gypsum) yanayopatikana kwa wingi katika Wilaya ya Mwanga, bado uwekezaji wake haujaweza kuwa na tija, zaidi ya kuchimbwa kwa kiwango cha chini na wachimbaji wadogo.

Kwa mujibu wa taarifa zinazohusu fursa ya uwekezaji kwenye madini, iliyowekwa katika tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, madini mengi hadi sasa hayajachimbwa ama yanachimwa kwa kiwango kidogo.

Zaidi taarifa hiyo imeeleza, madini ambayo yanachimbwa kwa wingi na yanaipatia halmashauri hiyo mapato kwa kiasi kikubwa ni madini ya ujenzi yanayotokana na uchimbaji wa mchanga.

Madini ya shaba yanapatikana kwa wingi katika maeneo ya Vuchama-Ndambwe katika Kata ya Shighatini na madini ya jasi yanayapatikana katika eneo la Njia Panda, Kata ya Kirya.

Uzalishaji wa madini ya gypsum nchini ni tani 354,000 na mahitaji ya soko ni tani 30,000 kwa mwezi katika viwanda vya saruji nchini.

Maeneo mengine yenye madini hayo ya gypsum ni Lindi, Itigi na Simiyu. Jasi inayopatikana Tanzania inatajwa kuwa ni ya ubora wa hali ya juu na nyingine kufikia kiwango cha ubora wa asilimia 98.

Aidha, madini ambayo yanachimbwa kwa wingi na yanayotegemewa kwa mapato ya ndani na halmashauri hiyo ni chokaa yanayochimbwa eneo la Kisangara katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mwanga.

Mengine ni udongo mweupe unaopatikana katika eneo la Lambo, Kata ya Shighatini na madini ya kokoto yanayopatikana kwa wingi ‘Kwanyange’ huko katika Kata ya Kivisini.

Kutokana na utajiri huo wa madini uliopo pia maeneo mbalimbali nchini, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, amekuwa akisisitiza kuwa ipo haja ya kuwahimiza wawekezaji au wachimbaji wenye leseni kuwekeza katika mitambo ya kuchenjulia madini ili kuyaongezea thamani, kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.