Chalamila amtumia salamu za pole Dk. Kebwe

12Aug 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Chalamila amtumia salamu za pole Dk. Kebwe

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe na familia zilizopoteza ndugu na jamaa katika ajali ya watu kuungua kwa mafuta iliyotokea juzi.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe

Chalamila alitoa pole hizo juzi wakati wa mkutano na wananchi wa Kata ya Utengule Usongwe, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kuongoza wakazi hao kusimama kwa dakika moja kuomboleza.

Alisema Mkoa wa Mbeya unaungana na mikoa mingine kuomboleza vifo vya watu zaidi ya 60 waliopoteza maisha baada ya kuungua moto walipokuwa wanachota mafuta baada ya lori lililokuwa limebeba bidhaa hiyo, kuanguka mkoani Morogoro.

Alisema taifa limepoteza Watanzania wengi ambao bado walikuwa wanahitajika na kuwaomba wafiwa wote kujifunga mkanda kwenye kipindi hiki cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao.

Kutokana na ajali hiyo, Chalamila alipiga marufuku wakazi wa Mbeya kusogelea ajali za malori ya mafuta ili kuchukua bidhaa hiyo kwa sababu ni hatari zinaweza kugharimu maisha yao.

Alisema umekuwa ni utamaduni kwa baadhi ya wananchi hususani madereva bodaboda kukimbilia kuiba mafuta pindi malori yanapoanguka na kusema ni hatari na waache mara moja.

"Tukiwa kwenye maombolezo ya kuwapoteza ndugu zetu waliopoteza maisha baada ya kuungua mafuta, nawasihi wana-Mbeya hususani madereva bodaboda kuacha tabia ya kukimbilia kuiba mafuta kwenye malori yaliyoanguka ili kuokoa  maisha yenu," alisema Chalamila.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Mchungaji Jacob Mwakasole, alisema taifa limepoteza nguvu kazi ya vijana wengi katika ajali ya moto na kusababisha majeruhi wengi.

Alipongeza jitihada za uokoaji zilizofanywa na Jeshi la Ukoaji na majeshi mengine, madaktari, taasisi na CCM Mkoa wa Morogoro kwa kuhamasisha wananchi kutoa damu kuokoa maisha ya majeruhi.

 

Habari Kubwa