Pinda azitaka taasisi kupambana na udumavu

12Aug 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Pinda azitaka taasisi kupambana na udumavu

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda, ameshauri taasisi zinazojihusisha na kilimo na lishe, vyuo na madaktari  kuandaa programu maalum ya kutoa elimu kwa jamii hasa kwa wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kutambua makundi yanayohitajika-

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda.

- ili kukabiliana na changamoto ya utapiamlo na udumavu.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akifunga Maonyesho ya Wakulima Nanenane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyohusisha mikoa saba kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya. Alisema licha ya mikoa hiyo kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, lakini kuna changamoto lishe hali inayosababisha udumavu kwa watoto wanaozaliwa.

Alisema ipo haja ya kuanzisha programu maalum ya kutoa elimu kwa jamii ili kumaliza changamoto ya utapiamlo na udumavu kwa watoto. "Haiwezekani mikoa hii ya Nyanda za Juu Kusini ikaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara vilevile ikaongoza kwa suala la udumavu ni aibu, lazima tuandae programu maalum ya kuisaidia jamii kuzingatia lishe bora," alisema Pinda.

Pia, aliwashauri kinababa ndani ya familia kuacha ubahiri wa fedha kwa kujitahidi kuwanunulia mahitaji ya nyumbani wake zao. Alisema wakati wanafikiria kuanzisha programu ya kukabiliana na udumavu pia kinababa wanapaswa kutambua wajibu wao kwa familia ikiwamo kuhudumia.