Wakulima wa mpunga walia uharibifu wa kweleakwela

12Aug 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
 Wakulima wa mpunga walia uharibifu wa kweleakwela

WAKULIMA wa mpunga katika Wilaya ya Mbarali mkoani  Mbeya, wameomba wataalamu wa kilimo kutafuta mbinu za kisasa kukabiliana na ndege aina ya kweleakwelea ambao kwa sasa ndiyo changamoto kubwa inayowakabili kutokana na kuharibu mazao yao yakiwa shambani.

ndege aina ya kweleakwelea

Ombi hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Mbeya wakati wa  kilele Siku ya Maonyesho ya Wakulima Nanenane. Mmoja wa wakulima hao, Batazan Lusigi, alisema ndege aina ya kweleakwelea wamewasababishia hasara kubwa wakulima wengi kwa sababu huvumia mashamba na kuharibu mazao.

Alisema wataalamu wanapaswa kubuni mbinu za kisasa za kuwadhibiti ndege hao kuokoa mazao shambani yasiharibiwe na ndege hao. "Msimu wa mavuno ukikaribia ndege hao jamii ya kweleakwelea kwa makundi huvamia mashamba ya wakulima   na kuharibu hali inayowasababishia hasara na kushindwa kupata mavuno yanayostahili, tunaomba wataalamu watusaidie suala hili kwa kuwa ni changamoto," alisema Lusigi.

Hata hivyo, Ofisa Kilimo mstaafu, Nuhu Mchame, ambaye kwa sasa anajihusisha na utafiti wa ndege hao, alisema kweleakwelea wanatabia ya kutembea katika makundi makubwa ya ndege zaidi ya milioni moja na wanapoingia shambani husababisha uharibifu mkubwa unaofikia asilimia 75 ya mazao shambani. Alisema ili kabiliana na uharibifu wa ndege hao lazima itafutwe njia ya kuwadhibiti ikiwamo kuwaua ili wasiendelee kuvamia mashamba ya mpunga na mazao mengine na kuwasababishia hasara wakulima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi, alisema halmashauri yake inashirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Wizara ya Kilimo, kusaidia wakulima kupunguza ndege hao kwa kuwaua kwa kuwamwagia sumu. Alieleza changamoto kuwa ni ndege hao kujificha na kuzaliana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambako sheria hairuhusu kuwaua wakiwa ndani ya hifadhi.

Mkuu wa wilaya hiyo, Reuben Mfune, aliwasihi wakulima kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji na kata wanaobaini makazi ya ndege hao ili wauliwe.Alikiri ndege hao kuwasababishia hasara kubwa wakulima na kwamba ni rahisi kuhama kwa sababu eneo kubwa linalolimwa mpunga ni tambarare.