Ndejembi  aiagiza Takukuru kuchunguza ujenzi sekondari

12Aug 2019
Ibrahim Joseph
KONGWA
Nipashe
Ndejembi  aiagiza Takukuru kuchunguza ujenzi sekondari

MKUU wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza mradi wa ujenzi wa majengo ya Shule ya Sekondari Kongwa kutokana na kuwapo na harufu ya ubadhirifu wa fedha.

MKUU wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi,

Sambamba na hilo, ameagiza kuhojiwa watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na makandarasi waliokuwa wakijenga majengo hayo kutokana na kukiuka miongozo ya serikali.  Ndejembi alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo.

Aliitaka taasisi hiyo kuchunguza kuanzia manunuzi ya vifaa mpaka bei ya vifaa na maduka yaliyotumika kununua vifaa hivyo, utaratibu wa kupitisha zabuni za ujenzi na thamani halisi ya gharama zilizotumika mpaka kufikia hatua ya majengo hayo.

"Ujenzi huu umekiuka utaratibu na kuisababishia serikali kuingia kwenye hasara kutokana na majengo kutokamilika wakati tayari Sh. milioni 290 zimeshatolewa,” alisema.

Alifafanua kuwa serikali ilipeleka Sh. milioni 150 kwa ajili ya mabweni, Sh. milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo na Sh. milioni 40 kwa ajili ya madarasa na samani zake, lakini baadhi ya majengo hayajakamilika na fedha zimeisha.  Alisema miongozo iliyowekwa na serikali ni kutumia mafundi wa ndani waliopo eneo husika na si kampuni za makandarasi.

Ndejembi alisema tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alishafanya ziara kwenye shule hiyo na kutoa maelekezo kuwa majengo yajengwe kwa kutumia utaratibu wa ‘Force account’, lakini hawajafuata wataalamu hao.

"Aliagiza kupelekewa taarifa ya ujenzi huu, lakini haijapelekwa jambo ambalo ni dharau haikubaliki, kwa ujumla sijaridhishwa na maendeleo ya ujenzi huu pamoja na thamani halisi ya fedha zilizotumika hapa,” alisema.

Aliwataja wanaotakiwa kuhojiwa na Takukuru ni ofisa manunuzi Yunus Mawaka, mhandisi wa ujenzi Wilaya hiyo, Christian Mlay, mkandarasi anayejenga bweni Majuto Mhando na mkandarasi anayejenga bwalo, Alfred Sembisa.

Alisema sababu za kutaka wahusika hao wakamatwe kuwa ni kutokana na kukiuka masharti ya fedha za ujenzi wa majengo hayo na kuwapo na harufu ya ufisadi. “Hawa wametumia utaratibu wa kushindanisha zabuni kwa makandarasi wakati sisi tunasema tunatumia mafundi waliopo eneo husika ili kupunguza gharama kubwa za ujenzi, wamekiuka masharti,” alisema. 

Aliutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kusimamisha kutoa fedha za ujenzi wa majengo hayo zilizobaki kiasi cha Sh. milioni 74 hadi uchunguzi huo utakapokamilika.

Ofisa Elimu Wilaya ya Kongwa, Honorata Kabunduguru, alisema serikali ilipeleka Sh. milioni 290 kwa ajili ya majengo matano ya shule hiyo. Alisema katika gharama hizo kila jengo lilitakiwa kukamilika pamoja na vifaa vyake mfano mabweni yalitakiwa kukamilika pamoja na kuwekewa samani zake ambazo ni vitanda na magodoro.

Hata hivyo, alisema kabla ya kuhamishiwa wilaya hiyo alikuwa Wilaya ya Mpwapwa ambapo fedha kama hizo zilizotumwa na kukamilisha ujenzi na kununua mahitaji yote kwa kutumia utaratibu wa ‘force account’ iliyokuwa chini ya kamati za ujenzi za shule husika.