Kituo maalum chatakiwa kwa kukusanya asali

12Aug 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Kituo maalum chatakiwa kwa kukusanya asali

SERIKALI imeombwa kuwatafutia wavuna asali kituo maalumu cha ukusanyaji zao hilo kutoka mashambani ili iwe rahisi kuwabaini baadhi ya watu wanaochakachua asali kabla haijaingia sokoni.

asali

Akizungumza na Nipashe katika viwanja vya Nanenane, mjasiriamali Christina Mushi, alisema ni muhimu serikali kuwa na kituo maalumu cha kukusanyia asali zao kwa ajili ya kuiuza kwa wafanyabiashara ili kuondokana na tabia ya baadhi ya watu kuchakachua na kuifanya asali kukosa viwango.

Aidha, alisema itawasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi kwa kuwa itapatikana asali yenye ubora.

“Kikiwapo kituo maalum ambacho kitakuwa kikipima kiwango na ubora wa asali hakuna atakayethubutu kuchakachua na badala yake italetwa asali iliyobora ambayo itapata soko kwa haraka,” alisema.

Alisema bila kufanya hivyo watu wachache wataendelea kuharibu zao hilo kutokana na tamaa ili wapate asali nyingi.

"Tunaiomba serikali ifanye jitihada ya kuanzisha kituo hiko tunahitaji kuingia katika soko la ushindani kwenye zao la asali kimataifa," alisema Christina.

Alifafanua zaidi ya kuwa hivi sasa ni vigumu kupata asali inayofanana kwa sababu kila mmoja anakusanya asali kivyake na kuileta sokoni jambo ambalo sio rahisi kuwabaini wanaochakachua.

Kadhalika, alilishukuru Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo  (SIDO) mkoani Dodoma ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inawafundisha wajasiriamali kutengeneza bidhaa zenye ubora unaotakiwa sokoni.

Aliwaasa wajasiriamali jijini Dodoma kujitokeza katika mafunzo yanayotolewa na shirika hilo ili wapate ujuzi ambao utawasaidia kuingiza bidhaa zao katika soko la kimataifa badala ya kuziuza mtaani pekee.

Naye mjasiriamali Hagai Wille, alisema hivi sasa vikundi vya wajasiriamali vinapaswa kujitoa kwenda kupata mafunzo yatakayowasaidia kukuza biashara zao.