Sheria ya kuchangia viungo mbioni kutungwa

12Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
IRINGA
Nipashe
Sheria ya kuchangia viungo mbioni kutungwa

SERIKALI ipo kwenye mchakato wa kutengeneza sheria ya kuchangia viungo ikiwamo figo ili kusaidia wagonjwa wenye matatizo hayo.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Daktari wa Afya ya Akili kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Omary Ububuyu, alipokuwa akitoa mada ya magonjwa yasiyoambukiza kwa waandishi wa habari za usalama barabarani, mjini Iringa.

Alisema robo tatu ya wagonjwa wamekuwa wakikosa ndugu wa kuwachangia figo na wengine wakishindwa kumudu gharama za matibabu hususan kwenye kusafisha damu.

Dk. Ububuyu alisema kwasasa zinatumika taratibu na kanuni zingine za kuchangia, lakini inakuja sheria maalum itakayofanya suala hilo liwe kisheria.

"Ili kila mtu atakayechangia alindwe na sheria, kama mtu ataona hajafanyiwa kitu sahihi kwa sheria hiyo ataenda kwenye bodi maalum ambayo atapata haki zake," alisema.

Hata hivyo, alisema ugonjwa wa figo unatokana na sababu mbalimbali zinazotokana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo na shinikizo la damu.

Alibainisha kuwa wagonjwa ambao wamesajiliwa kutokana na figo kutofanya kazi nchini kwa sasa ni takriban 851 kwenye hospitali za kanda, rufani na taifa.

"Hawa wanahitaji huduma ya figo bandia, wanahitaji mashine iwasaidie kusafisha damu au kupandikizwa figo, na gharama za matibabu yake ni kubwa hasa katika kusafisha damu," alisema.

Aliongeza kuwa: "Kwa session moja mgonjwa wa kusafishwa damu itamgharimu mtu Sh. 250,000 hadi Sh. 300,000 na anatakiwa awe na session tatu kwa wiki moja, hivyo ndani ya mwezi Sh. milioni 3-4, hata uwe Gavana wa BoT ni ghali sana."

Alisema kwa mwaka mgonjwa atalazimika kutumia Sh. milioni 36-48, na kama kisukari na shinikizo la damu vitaendelea kushambulia itasababisha figo kushindwa kufanya kazi.

Mtaalamu huyo alisema takriban Sh. bilioni 26 hadi 40 zinahitajika kwa mwaka kwa wagonjwa wa figo kwa ajili ya kusafishwa damu na asilimia 30 ya wagonjwa wanashindwa kumudu gharama hizo na serikali inalazimika kubeba mzigo.

"Hizo gharama ni kubwa hata zikiingizwa kwenye bima kwa asilimia 100 itahatarisha mfuko, ni changamoto, mpaka sasa wagonjwa 40 wamepandikizwa, tuhamasishe wananchi kuchangia figo," alisema.

Kwa magonjwa yasiyoambukiza, alisema yanaendelea kuongezeka nchini na kuchangia vifo kwa asilimia 33.

"Pia takwimu za kidunia zilizotolewa na WHO, magonjwa yasiyoambukiza yanaongoza kwa kuua watu wengi zaidi mpaka sasa takwimu zinaonyesha kwamba kwa mwaka 2012 watu milioni 16 wamefariki dunia kutokana na vifo visivyotarajiwa.

"Vifo visivyotarajiwa ni vile vya kabla ya miaka 70 na asilimia 82 ya vifo hivyo vimetokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza," alisema.

Alibainisha kuwa upatikanaji wa dawa ni changamoto na dawa zake ni za gharama kubwa na mzigo kwa serikali na kwa watu binafsi.

"Watu wengi wanachelewa kupata tiba ya magonjwa kama vile sukari, moyo au saratani kutokana na kuchukua muda mrefu kugundulika," alisema.

Vile vile, alisema katika utafiti uliofanywa na STEPPS ulioshirikisha Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Wizara ya Afya kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, asilimia 25 ya waliopimwa wana changamoto ya shinikizo la juu la damu na kwa bahati mbaya asilimia 68 ya watu hawakuwahi kujua kabla kuwa wanaumwa.

"Katika kila watu wawili kati ya watatu hawajui kama wana tatizo la shinikizo la damu, magonjwa mengine kama selimundu, Tanzania inaingia katika nchi 10 duniani zenye tatizo hilo, na kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa sita wana tatizo la selimundu," alisema.

Alifafanua kuwa vipo vihatarishi vingi vya magonjwa hayo ikiwamo lishe duni kwa kula chakula ambacho hakipo kwenye mpangilio unaotakiwa, uzito uliopitiliza, mtindo wa maisha ikiwamo kubweteka kutoshughulisha mwili.

"Vingine ni vilevi hata mwanamke kipindi cha ujauzito hatakiwi kutumia pombe kabisa kwa kuwa anamuweka mtoto kwenye hatari katika ukuaji wake," alisema.

Mikakati ya serikali

Alisema magonjwa hayo kutokana na kuwa na gharama kubwa serikali inajipanga kutengeneza mpango maalum wa kudhibiti na kuzuia magonjwa hayo.

"Pia tutakuwa na wiki ya magonjwa yasiyoambukiza tuunganishe nguvu zote kukabiliana nayo, kutakuwa na kampeni maalum kama ilivyofanyika kwa magonjwa mengine, itafanyika Novemba 9 hadi 16 na mwaka huu itafanyika Dodoma," alisema.

Habari Kubwa