Tanzanite mabingwa wapya Cosafa U-20

12Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tanzanite mabingwa wapya Cosafa U-20

TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake ya umri chini ya miaka 20 (Tanzanite), imefanikiwa kuutwaa ubingwa wa mashindano ya Cosafa baada ya kuwafunga wenzao wa Afrika Kusini mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Wolfson mjini Port Elizabeth.

TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake ya umri chini ya miaka 20 (Tanzanite)

Mabingwa hao wapya walienda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0 katika mchezo huo uliochezwa jana mchana nchini Afrika Kusini.

Tanzanite ambayo ni timu mwalikwa katika mashindano hayo, imetwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza ikiwa na Kocha Mkuu Mtanzania Bakari Shime ambaye anasaidiana na kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Wanawake maarufu, Twiga Stars, Edna Lema.

Bao la kwanza la Tanzanite lilifungwa na mshambuliaji wa Simba Queens, Opa Clement dakika ya 24 katika mchezo huo ambao timu zote zilicheza kwa kukamiana.

Zikiwa zimebakia dakika tatu ili mchezo huo umalizike, mshambuliaji, Protasia Mbunda alifunga bao la ushindi na kuinyamazisha Zambia ambayo iliwafungwa Tanzanite katika hatua ya makundi kwa mabao 2-1.

Tanzanite iliyokuwa katika Kundi B ilitinga hatua ya fainali baada ya kuwachapa wenyeji Afrika Kusini mabao 2-0 wakati Zambia yenyewe iliwafunga Botswana goli 1-0.

Shime alisema kujituma na kutokata tamaa kwa wachezaji wake ndio kumeifanya timu hiyo ipate ushindi katika michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.

Kocha huyo aliongeza kuwa, ushindani ulioongezeka kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania na Ligi Daraja la Kwanza, ndio imechangia kupata wachezaji wenye uwezo mzuri na wenye kiu ya mafanikio.

Kikosi cha Tanzanite kinatarajia kurejea nchini leo huku dada zao Twiga Stars wakijiandaa kuelekea Nairobi kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya wenyeji Kenya utakaochezwa Alhamisi Agosti 15 mwaka huu.