Kaseja afunguka AS Kigali itafia Dar

12Aug 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kaseja afunguka AS Kigali itafia Dar

KUFUATIA sare tasa katika mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Kigali, Nahodha wa Klabu ya KMC FC, Juma Kaseja amesema wana nafasi nzuri ya kurekebisha makosa yao na kushinda mechi ya marudiano wiki mbili zijazo hapa nchini.

Nahodha wa Klabu ya KMC FC, Juma Kaseja

Akizungumza na Nipashe juzi kutoka Kigali, Kaseja alisema kwa ujumla timu yao ilijitahidi kutokana na ushindani mkali katika mechi hiyo.

"Japokuwa tumepata sare ugenini bado tuna dakika 90 ambazo tutazitumia vizuri kwenye mchezo wetu wa marudiano,"alisema Kaseja.

Hata hivyo, aliongeza kuwa kikosi chao kilichocheza kilikosa baadhi ya nyota wao kutokana na vibali vyao vya kimataifa (ITC) kuchelewa, lakini akasifu juhudi zilizoonyeshwa na wachezaji waliocheza.

Kaseja pia aliwashukuru Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa waliowaonyesha wakati wakiwa Rwanda na kuwaahidi kufanya makubwa kwenye mechi ijayo hapa nchini.

Endapo KMC itafanikiwa kusonga mbele, itakutana na mshindi kati ya Proline FC ya Uganda anapotokea kocha wao, Jackson Mayanja na Masters Security Services ya Malawi.

Habari Kubwa