Simba, Yanga inawezekana zikijipanga dk. 90 za pili Caf

12Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga inawezekana zikijipanga dk. 90 za pili Caf

MWISHONI mwa wiki wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Simba, Yanga na KMC walilazimishwa sare katika mechi zao za awali kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba na Yanga zinapeperusha bendera ya nchi kwenye Ligi ya Mabingwa wakati KMC na Azam FC ambayo jana ilikuwa dimbani dhidi ya Fasil Ketema ya Ethiopia, zinabeba jukumu hilo upande wa Kombe la Shirikisho.

Katika michuano hiyo inayoandaliwa na kuratibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Simba ikiwa ugenini nchini Msumbiji ililazimishwa sare tasa dhidi ya UD Songo.

Na kwa upande wa Yanga ikiwa nyumbani katika Uwanja wa Taifa, ilibidi kusubiri hadi dakika ya 84 kuweza kusawazisha kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Patrick Sibomana wakati ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Miamba ya Kinondoni, KMC nayo ilitoka sare tasa ugenini nchini Kigali dhidi ya AS Kigali anayoichezea nyota wa zamani wa Yanga na Simba, Harouna Niyonzima.

Kwa ujumla matokeo hayo si mabaya sana kwa timu zote, ingawa kwa Yanga yanaweza kuwa si mazuri sana kwani kutokana na mfumo wa michuano hii inayochezwa nyumbani na ugenini kuruhusu bao la nyumbani linagharimu mechi ya marudiano.

Hata hivyo, kama ambavyo Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera alivyosema mara baada ya mechi kuwa timu yake inazidi kuimarika na anaweza kupata matokeo ugenini hata kwa kushinda 2-1, ndivyo ambavyo na sisi tunatamani kuona hilo likitokea.

Tunazidi kupata matumaini hayo, hasa kwa kuzingatia kauli ya Zahera kuwa hawana cha kupoteza wiki mbili zijazo ugenini na kwamba watakwenda kushambulia mwanzo mwisho huku akiahidi kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza hususan katika safu ya ushambuliaji.

Lakini pia kwa upande wa Simba na KMC nazo hazipaswi kubweteka sana kwani matokeo ya sare tasa ugenini,  yanahitaji umakini sana kwenye mechi ya marudiano nyumbani kwa kuhakikisha mgeni hapati bao. Hivyo, kwa ujumla kinachotakiwa kwa Simba na KMC na hata Azam, ni kuhakikisha zinatumia vema faida ya uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wao.

Lakini pia, tunatambua kutopata matokeo kwa timu hizo kunaweza kuchangiwa na ukweli kwamba hizo ndizo mechi zao za kwanza za kimashindano msimu huu.

Na kwa namna zilivyoweza kucheza kwa kasi, hilo linatupa matumaini kwamba mechi zijazo za marudiano zitakuwa zimeimarika zaidi na kuweza kupata matokeo hususan kwa Yanga ambayo itakuwa ugenini.

Kinachotakiwa ni kutambua kuwa hizo ni dakika 90 za awali bado zingine kama hizo za kuweza kupata matokeo na kusonga raundi ya kwanza ya michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Nipashe tunaamini makocha wa timu zote zinazoipeperisha bendera ya nchi kwenye michuano hiyo  wamebaini kilichowanyima ushindi na watakwenda kukifanyia kazi kabla ya marudiano na kuweza kusonga mbele.

Kuna wiki mbili za kujipanga upya kabla ya kurudiana mwezi huu kati ya Agosti 23-25, hivyo tunataka kuona timu zote nne zikisonga mbele na hilo litawezekana tu kama kutafanyika maandalizi ya kina, huku mashabiki wakiungana na timu zao dimbani kwa kuzishangilia mwanzo mwisho. Kila la heri wawakilishi wetu katika dakika 90 za pili Caf.

Habari Kubwa