Tanzanite wameweza Cosafa,  serikali, TFF iwamulike zaidi

12Aug 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tanzanite wameweza Cosafa,  serikali, TFF iwamulike zaidi

IKIWA ni timu alikwa kwenye michuano ya (COSAFA), timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake wa umri chini ya miaka 20, imetwaa ubingwa na michuano hiyo kwa kuichapa timu ya Taifa ya Zambia mabao 2-1.

Michuano hiyo ilikuwa ikifanyika nchini Afrika Kusini, na mechi hiyo ya fainali ilichezwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Wilfson Port Elizabeth.

Chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime, mabao ya Tanzanite yalifungwa na Opa Clement dakika ya 24 na Protasia Mbunda dakika tatu kabla ya pambano kumalizika.

Ilikuwa ni hoi hoi nderemo na vifijo kwa akina dada hao wa Kitanzania mara baada ya filimbi ya mwisho ya mechi hiyo, huku wakipewa sapoti na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo waliokuwa wakishangilia kwa nguvu, wakiwa wamebeba bendera ya Tanzania.

Uchezaji na nyimbo za Kibongo zilizokuwa zikiimbwa na akinadada hao, benchi la ufundi pamoja na Wabongo waishio Sauzi vilikuwa ni burudani tosha.

Pongezi kubwa kwa kocha mkuu, viongozi walioandamana na timu hiyo, wachezaji pamoja, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Watanzania wote kwa ujumla.

Kwa mara nyingine tena imedhihirisha kuwa kwa sasa Tanzania imeanza tena kuanza kupiga hatua kwenye masuala ya michezo.

Miaka kadhaa nyuma, Tanzania haikuwa na chochote cha kujivunia kwenye nyanja za michezo kiasi cha hata Wabongo kushindwa kutamba wanapokwenda kwenye nchi zingine.

Tangu Hassan Mwakinyo alipoanza kumchapa bondia mzungu nchini Uingereza, Simba kufika robo fainali Ligi ya Mabingwa, Taifa Stars kufanikiwa kufuzu AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40, pamoja na ushindi wa majuzi wa Taifa Stars wa kutafuta kufuzu CHAN, nchi imekuwa na maendeleo mazuri na hata mwelekeo umeanza kuonekana kuwa mzuri.

Hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliliongelea hilo kwenye tamasha la Simba Day, lakini pia akitamka kuwa serikali imeruhusu uwekezaji kwenye klabu kwa ajili ya kuzifanya kuwa nzuri kiuchumi na kuzidi kufanya vema kimataifa na kuiletea sifa nchi.

Pamoja na pongezi, lakini kinachotakiwa sasa ni kutojisahau kwani akina dada hao ndiyo wanaokwenda baadaye kuunda kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars hivyo inafaa waangaliwe kwa jicho pana zaidi.

Tatizo kubwa ninaloliona kwenye timu za vijana za wanaume na wanawake Tanzania, huwa na wachezaji wenye vipaji, lakini wengi hupotelea kati na huwa hawajulikani wanapoenda.

Watanzania tusipende tu kuwapokea kwa kishindo na mbwembwe nyingi wanapokuwa wanamichezo wameshinda na baada ya hapo wanaachwa waendelee na maisha yao, hapo ndipo tunapowapoteza.

Uchunguzi mdogo unaonyesha kuwa wengi wao wanashindwa kuendelea na vipaji vyao kutokana na wazazi wao kuwataka wakazanie zaidi masomo kuliko michezo, wengine wanaachana na soka na kuanza kusaka pesa kwa sababu ya matatizo ya kifamilia na wengine wanalewa sifa na kushindwa kujitambua na kujitunza hadi kudumaza vipaji vyenyewe.

Kwa kinadada hawa, inabidi TFF na serikali kupitia wizara husika kukaa chini na kufanya mikakati ya kuwasaidia mabingwa hawa ili kulinda vipaji vyao visaidie taifa mbele ya safari kama vilivyofanya huko Sauzi.

Kwanza kabisa wawe wanakutana mara kwa mara kwa ajili ya mazoezi, lakini pia kuwasaidia kwenye masomo yao kama vile ada na mambo mengine ambayo familia zao zinashindwa kutatua, na kupewa ushauri nasaha ni jinsi gani ya kujitambua na kujitunza ili kuepuka kufifisha vipaji vyao.

Habari Kubwa