Ajali ya Morogoro, amani vyatalawa Eid 

13Aug 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ajali ya Morogoro, amani vyatalawa Eid 

WAUMINI wa dini ya Kiislamu wametakiwa kujifunza kupitia tukio la moto lililotokea mkoani Morogoro na kuishi maisha yanayompendeza Mwenyezi Mungu kwa kuwa hawajui siku ya mwisho ya maisha yao.

Rais wa Zanzibar, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein

Sambamba na hilo, wametakiwa kuendelea kuwaombea viongozi wakuu wa serikali ili wawe na busara na hekima katika kuliongoza vyema taifa.

Wakati hayo yakihimizwa, Rais wa Zanzibar, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka waumini wa dini hiyo na Watanzania kwa ujumla kudumisha amani ambayo ni tunu muhimu kwa taifa la Tanzania.    

Akitoa mawaidha katika ibada ya Sikukuu ya Eid el Hajj, iliyofanyika katika msikiti wa Gadafi jijini hapa, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban, alisema  Waislamu wanatakiwa kujifunza kupitia tukio hilo kwa kuishi katika misingi inayompendeza Mungu ili kujiandaa na safari yao ya mwisho katika maisha yao.

"Tunaona kama ndugu zetu waliokufa pale Msamvu, Morogoro kutokana na ajali ya lori la mafuta ambavyo waliteketea kwa moto, hivyo ndivyo ilivyo hata kwetu kwani hatujui kifo chetu kitakuwaje. Ni lazima tujiandae kila wakati kwani Mwenyezi Mungu anatoa hukumu yake baada ya sisi kufa," alisema.

Pia aliwataka waendelee kuwaombea viongozi kwa kuwa bila viongozi wakuu wa nchi kuwa na busara, hekima na afya njema, hawawezi kuliongoza taifa, hivyo kuchangia kwa baadhi ya mambo kutokwenda sawa.

"Lazima tuendelee kuwaombea hawa viongozi wetu kwani bila wao kuwa na vitu hivi, taifa haliwezi kusonga mbele. Lazima tuendelee kuwaombea kwa Mungu ili  wayafanikishe yale yote ambayo wameyapanga kwetu," alisema.

Aliwataka waumini wa kiislamu kuwa na umoja kwa kufanya mambo kwa kushirikiana ili kujikwamua kiuchumi.

"Ndugu zangu Waislamu, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo yatupasa kushirikiana ili kutoka hapa tulipo kama mnavyoona kwa kiongozi wetu Mufti (Sheikh Mkuu wa Tanzania) ambavyo ameondoa migogoro iliyokuwapo awali baina ya makundi mbalimbali ya Waislamu nchini," alisema.

Aidha, aliwataka Waislamu kuacha tabia ya kuitumia siku ya Eid el Haji kuwa ni sehemu ya kulewa pombe kupita kiasi au kuwa wakorofi wa kupindukia.

Katika hatua nyingine, Sheikh wa Wilaya ya Bahi, Suleman Twalib, aliwataka Waislamu kuitumia sikukuu hiyo kuwakumbuka watu wasiojiweza wakiwamo yatima, wajane na wazee.

Sheikh Twalib aliwataka kuhakikisha wanatumia furaha hiyo ya sikukuu kujumuika na watu wa jamii hiyo ambao mara nyingi wamekuwa wakisahaulika.

Alisema inasikitisha kuona baadhi ya waumini wa Kiislamu inapofikia siku kama hiyo, wako tayari kutumia mali na fedha zao kwa anasa huku wakiwaacha wasiojiweza bila kuwasaidia.

Pia aliwataka waumini wa wilaya hiyo wenye sifa ya kuwa viongozi katika nafasi za uenyekiti wa serikali za mitaa kujitokeza kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

BAKWATA WATOA POLE

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata)  Mkoa wa Singida limetoa pole kwa Rais john Magufuli kutokana na vifo vya watu 71 waliofariki dunia kwa kuungua moto mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki.

Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Burhan Mlau, alitoa pole hiyo katika sala ya Eid Al Haji iliyofanyika jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Sumaye, mkoani hapa.

"Tunampa pole Rais wetu kwa msiba huu mkubwa tulioupata pamoja na wafiwa na tunawaombea majeruhi wote wapate nafuu na kurejea katika shughuli za ujenzi wa taifa" alisema Mlau.

Katika sala hiyo, Mlau aliwataka Waislamu mkoani hapa kuwa kitu kimoja na kuondoa utengano kupitia taasisi zao mbalimbali badala ya kutengana.

"Nawaombeni ndugu zangu Waislamu tuendelee kushikamana na kupendana kupitia taasisi zetu jambo ambalo litadumisha uislam wetu na kumpendeza Mwenyezi Mungu," alisisitiza.

Katika kusherehekea sikukuu hiyo Mlau aliwaomba waislam wa mkoa huo kusherehekea kwa utulivu  na amani huku wakiwaangalia watoto wao kwa ukaribu.

Imeandikwa na Paul Mabeja na Peter Mkwavila, DODOMA; Doto Mwaibale, SINGIDA na Gwamaka Alipipi, DAR. Habari zaidi Uk. 23

Habari Kubwa