Jafo Ataka Amani

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jafo Ataka Amani

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo, alisema Tanzania haiwezi kwenda katika uchumi wa kati bila  kuwa  na amani.

Seleman Jaffo

Jafo alisema hayo jana katika Baraza la Eid na sala ya Eid el-Hajj kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya Masjid Kibadeni Chanika jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa mgeni rasmi.

“Ajenda ya amani, hakuna yeyote mwingine ambaye atafurahia kuona nchi inakosa amani. Tunapaswa kujielekeza  kwenye amani na ukipoteza amani umevunja amani ya nchi, Watanzania tuendelee kuliombea taifa,” alisema Jaffo.

Alisema ufisadi, dhuluma na chuki vinajenga matabaka baina ya watu, lakini Rais Magufuli amejitahidi kuviondoa tangu alipoingia madarakani na ndiyo maana aliamua kuanzisha Mahakama ya Mafisadi ili watu wabadilike kimawazo na kifikra.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zubeiry, alisema Bakwata haitavumilia mtu atakayeivunjia amani, heshima na kwamba itahakikisha chombo hicho kinaheshimiwa na kila Mwislamu.

Kwa upande wake, Kaimu Sheikk wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Kitogo, aliwataka Waislamu kuwa kitu kimoja, waungane, washikamane na wadumishe amani

Naye Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Jabir Mruma, alisema: “Tunakerwa na migogoro inayotokea ndani ya misikiti. Malizeni haraka, msipomaliza kwa haraka migogoro yenu Bakwata litaingilia kati. Tunataka migogoro yote imalizwe ngazi ya chini kabla haijaletwa katika ngazi ya juu.”

Habari Kubwa