Kigogo CCM ashukia waliochoma nyumba

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
SIMIYU
Nipashe
Kigogo CCM ashukia waliochoma nyumba

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameunga mkono uamuzi wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, kusitisha operesheni ya kuwaondoa na kuwachomea nyumba na mazizi wananchi wa Kijiji cha Vilimavitatu wilayani Babati mkoani Manyara.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally

Amesema kitendo kilichofanywa na viongozi hao wa wilaya ni cha kinyama kwa kuwa kimefanywa dhidi ya raia wasiokuwa na hatia.

Akizungumza na wanachama wa CCM wilayani Meatu mkoani Simiyu kwenye ziara yake mkoani humo mwishoni mwa wiki, Dk. Bashiru alisema operesheni hiyo iliyoendeshwa na uongozi wa Wilaya ya Babati imesababisha familia nyingi kuishi bila makazi.Alisema operesheni hiyo imefanyika wakati tayari Rais John Magufuli alishaunda kamati ya mawaziri wanane akiwamo Mpina kushughulikia changamoto za wananchi wanaoshi jirani na maeneo ya hifadhi na hajatoa uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo.Alisema ni lazima viongozi wa chama hicho waliopewa dhamana ya kusimamia serikali, kufuatilia kwa karibu maagizo yote ya Rais ambaye ni Mwenyekiti wa chama.

Tayari Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mpina amesitisha operesheni ya kuwaondoa na kuwachomea nyumba, mazizi ya mifugo na makambi ya uvuvi wananchi wa Kijiji cha Vilima vitatu na kuunda timu ya wataalamu kutoka wizara nae kufuatilia utekelezaji wa operesheni hiyo na kuwasilisha ripoti hiyo serikalini kwa uamuzi zaidi.

"Inawezekanaje mkuu wa nchi ameelekeza tulieni kwanza tufanye utafiti, tufanye uchambuzi, msifanye lolote mpaka tutakapokuwa tumetoa maelekezo halafu mtu anageuka, aliyeteuliwa na Rais. huyo huyo anavuruga utaratibu," Dk. Bashiru alihoji.“Maagizo ya Rais ni maagizo ya mwenyekiti, ukishasikia ameagiza Rais na ni Rais wa CCM, wewe hayo ni maagizo ya mwenyekiti wako, anza kutekeleza ndiyo namna ya kukipa heshima chama chetu, tukianza kupishana kati ya serikali na chama katika mambo ya msingi, hatutaweza kupata uhalali wa kuongoza nchi yetu."

Ilielezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wiki iliyopita kuwa operesheni hiyo ya Babati iliyofanyika Julai mwaka huu,  imesababisha wananchi wengi kukosa mahali pa kuishi  kutokana na nyumba zao kuchomwa moto na sasa wanaishi chini ya miti.Pia, ilielezwa na wizara hiyo kuwa mifugo ya wananchi hao imekuwa ikivamiwa na wanyama wakali na mingine kupotea baada ya mazizi kuchomwa huku shughuli za uvuvi nazo zikisimama baada ya makambi na zana za uvuvi kuteketezwa.

Habari Kubwa