Rais wa Afrika Kusini kuwasili leo

13Aug 2019
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rais wa Afrika Kusini kuwasili leo

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ataingia nchini leo kwa ziara ya siku mbili na baadaye kushiriki katika mkutano wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Makonda alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa rais huyo, jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa viongozi wa SADC unatarajiwa kuanzia Agosti 16 na Rais Dk. John Magufuli ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo atakabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob.

Makonda alisema wiki hii itakuwa ya maandalizi ya kuwapokea marais wa nchi za Jumuiya hiyo watakaohudhuria mkutano huo. Viongozi wa nchi 16 wanatarajiwa kuingia nchini kushiriki mkutano huo.

Pia, Makonda alisema ujio wa viongozi hao utatoa fursa kwake kuuliza jinsi nchi hizo zinavyowashughulikia wanaume wanaowaumiza wanawake.

Alisema wanawake wengi wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakilalamikia kuumizwa na wanaume kwa kutapeliwa na kuachwa na majeruhi moyoni mwao.

Alisema akiwa kama Mkuu wa Mkoa, hawezi kuwaongoza watu wenye kuumizwa hivyo atakwenda kuwashughulikia na kwamba kupitia mkutano huo wa SADC watapata uzoefu jinsi wao wanavyoshughulikia wanaume wa aina hiyo.

"Tuna mpango wa kukutana na kinadada wote walioumizwa na ahadi za kuolewa, lakini wakaachwa ili kujadiliana kwa kina namna gani ya kuwashughulikia wanaume hao, lakini pia tutajifunza kwa wenzetu wa SADC sheria zao zinafanyaje kuwashughulikia wanaume wadanganyifu," alisema na kuongeza:

“Lengo ni kuepusha kinadada wasiingie kwenye uhusiano wa kuumizwa, lakini pia itasaidia kuondoa ndoa za kimya kimya, wageni wetu watatuambia huko kwa Mfalme Mswati wanafanya utaratibu gani, Zimbabwe wanafanyaje ili tuone ni njia gani ya kuwaondoa kinadada wasiendelee kuumizwa,” alisema Makonda.

Pia, Makonda alisema kuna mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.

Wakati huo hui, Mkutano wa Mawaziri wa SADC unatarajiwa kuanza leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, atakabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa ngazi za mawaziri.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa pikipiki mpya zinazotarajiwa kutumiwa katika mapokezi ya viongozi na wakuu wa nchi na serikali wa SADC kwaajili ya kuhudhuria mkutano huo unaoendelea jijini Dar es Salaam, Prof. Kabudi, alisema serikali imekuwa ikiendelea na maandalizi mbalimbali ya mapokezi ya viongozi hao ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri yakiwamo magari na pikipiki na hoteli watakazofikia viongozi hao.

Pia Prof. Kabudi kwa niaba ya serikali, ameeleza kuridhishwa na kufurahishwa kwa namna vyombo vya habari nchini vinavyoripoti kizalendo mkutano unaoendelea wa SADC jambo ambalo limeongeza uelewa wa wananchi kuhusu Jumuiya hiyo na kuvitaka kuendelea kufanya hivyo katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya nchi.

Katika tukio jingine, Waziri Prof. Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Denmark Nchini Tanzania Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet.

Katika mazungumzo yao Prof. Kabudi alimhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chake cha uwakilishi nchini huku Balozi Mteule Mette Norgaard Dissing-Spandet akiipongeza serikali kwa mageuzi ya haraka inayoyafanya ili kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na kuongeza uwajibikaji serikalini.

Habari Kubwa