Serikali mbioni kubadili mitaala elimu ya ualimu

13Aug 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali mbioni kubadili mitaala elimu ya ualimu

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema inakusudia kufanya marekebisho ya mitaala ya elimu ya ualimu ili iendane na mabadiliko mbalimbali.

Dk. Leonard Akwilapo

Mabadiliko hayo ni pamoja na mitaala ya shule za msingi na sekondari ambayo yalianza kutumika mwaka 2015.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Leonard Akwilapo, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa elimu ya ualimu, waliokutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa maoni ya kuboresha usimamizi na maendeleo ya maboresho ya mitaala ya ualimu.

Alisema mtaala wa mafunzo ya ualimu uliopo sasa ni wa zamani  akitolea mfano wa mafunzo ya ualimu kwa walimu wa diploma ambao ni wa mwaka 2008, huku ngazi ya cheti ukiwa wa mwaka 2009 hivyo kutoendana na mtaala mpya wa elimu msingi ambao unazingatia ufundishaji wa KKK.

"Elimu ni suala la kitaifa hivyo serikali haiwezi kujifanya haisikii, jamii inasema nini ndio maana kikao cha wadau kimeitishwa na pia Waziri wa Elimu yupo mbioni kuitisha mkutano wa wadau kwa lengo la kupata maoni ya namna bora ya kuboresha elimu," aliongeza Dk. Akwilapo.

Pia Katibu Mkuu huyo aliwataka wadau hao kutumia mkutano huo kujadili na kutafakari kwa kina mfumo wa maandalizi ya walimu nchini kwa kuzingatia mada ya Usimamizi na Maendeleo ya Elimu ya Ualimu, Fursa na Changamoto pamoja na upimaji na tathmini yake.

"Tumieni mkutano huu vizuri na mambo mtayakojadili yajikite katika kuona ni namna gani mnaboresha mahiri zinazohitajika kwa mwalimu, ama mkufunzi, mazingira na miundombinu wezeshi, uongozi na usimamizi wa mafunzo, upimaji na tathmini ya mafunzo pamoja na maendeleo endelevu ya mwalimu," alisisitiza Dk. Akwilapo.

Naye Kamishna wa Elimu, Dk. Lyabwene Mtahabwa, alisema  mkutano huo wa wadau wa  elimu utachochea mabadiliko katika sekta nzima ya elimu kwa kuwa ili kufanikiwa katika sekta hiyo ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wadau wa elimu.

"Tumekutana kwa ajili ya kuongelea moyo wa taifa letu, elimu ni moyo wa taifa unaposema elimu unapozungumzia elimu ya ualimu katika kuleta mabadiliko ya sekta nzima ya elimu," aliongeza Dk. Mtahabwa.

"Unaweza kujenga shule nyingi, ukawa na vifaa vya kutosha, lakini kama hauna walimu bora ni kazi bure hivyo tunataka walimu wawe na waledi, wawe kioo cha jamii kuanzia uvaaji wake, kutembea, kuongea na namna anaivyoishi shuleni na hata kijijini awe mfano wa kuigwa katika jamii," alisema.