Mahakama Kuu yakubali viongozi EAGT kushtakiwa

13Aug 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mahakama Kuu yakubali viongozi EAGT kushtakiwa

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imekubali kuwa viongozi wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God (EAGT) wanastahili kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za kanisa ikiwamo ukwepaji kodi kwa kuingiza magari kinyume cha taratibu na  uvunjaji wa Katiba ya kanisa hilo

Viongozi hao ambao ni walalamikiwa katika kesi hiyo ni wadhamini wa kanisa hilo, Mchungaji Christomoo Ngowi na Mchungaji Asumwisye Mwang'mbola (kwa sasa marehemu).

Wengine ni Askofu Mkuu Brown Mwakipesile, Katibu Mkuu, Mchungaji Leonard Mwizarubi na Mweka Hazina Mchungaji Praygod Mgonja, wote wa kanisa hilo.

Uamuzi huo umetolewa Agosti 9, mwaka huu na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji Leila Mgonya, baada ya kutupilia mbali hoja tano za pingamizi la awali la walalamikiwa wakidai kwamba hawastahili kufunguliwa kesi na kushtakiwa kama watu binafsi katika maombi madogo ya madai namba 54/2019.

Walalamikaji ni wachungaji Yared Lesilwa, Gilbert Weja na Petrol Kapama kwa niaba ya wachungaji wengine 546 nchini, wamefungua maombi hayo Februari 11, mwaka huu na kupangiwa kusikilizwa mbele ya Jaji Mgonya.

Walalamikaji kupitia Wakili Edwin Swalle, wamefungua maombi hayo wakiiomba mahakama kuruhusiwa kuwashtaki viongozi hao kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za kanisa ikiwamo ukwepaji wa kodi kwa kuingiza magari kinyume cha taratibu.

Ilidaiwa kuwa magari hayo yalipata msamaha wa kodi wa serikali wakati hayapo kwenye orodha ya mali za kanisa jambo ambalo ni uvunjifu wa katiba, kuwafukuza wachungaji bila ya kufuata katiba ya kanisa na sheria za nchi.

Vile vile, walalamikiwa kupitia wakili Didas Kanyambo, walipinga maombi hayo wakidai kuwa hawastahili  kushtakiwa kwa mashtaka hayo ila bodi ya wadhamini ya kanisa hilo ndiyo ishtakiwe siyo wao kama viongozi kwa majina yao.

Hata hivyo, mahakama iliangalia kama wadaiwa hao wanastahili kushtakiwa binafsi ama bodi ya wadhamini ya kanisa hilo, ilijiridhisha kwamba wanastahili kufunguliwa mashtaka na kuburuzwa mahakamani.

Wakili Swalle, alidai kuwa kwa kuwa mahakama imekubali maombi yao walalamikaji wanatarajia kuwafungulia mashtaka ya ubadhirifu wa mali za kanisa, ukwepaji wa kodi kwa kuingiza magari kinyume cha utaratibu na uvunjaji wa katiba ya kanisa hilo.

Katika madai ya msingi, walalamikiwa hao  wanatuhumiwa kutengeneza Tin namba zaidi ya nne kwa jina la kanisa na kwamba kwa mujibu wa sheria, taasisi inatakiwa kuwa na Tin namba moja tu.

TIN zinazosemekana zimesajiliwa na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa jina la EAGT ni pamoja na; TIN No. 1000932326 kwa jina la Temeke Evangelistic Assemblies of God.

TIN No. 103600766 kwa jina la; Evangelistic Assemblies of God (T) ambayo inadaiwa kutumika kuingiza magari sita.

TIN No. 114558796 kwa jina la Evangelistic Assemblies of God Tanzania ambayo anadaiwa kutumika kuingiza magari matano.

TIN No.101060063 kwa jina la Evangelistic Assemblies of God CD ambayo inadaiwa kutumika kuingiza magari 15

TIN No. 103947200 kwa jina la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) ambayo inadaiwa kuwa ni halali lakini inadaiwa kuingiza magari 52.

Ilidaiwa kuwa kabla  ya kufunguliwa kwa maombi hiyo walalamikaji walipata ridhaa na baraka kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Adelardus Kilagi.

Habari Kubwa