Sera yakwamisha viuadudu kupulizwa

13Aug 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sera yakwamisha viuadudu kupulizwa

TATIZO la kisera nchini lilikwamisha matumizi ya dawa ya viuadudu inayozalishwa na Kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluilui vya mbu cha Tanzania Biotech Product(TBPL).

Dawa hiyo yenye uwezo wa kuua mazalia ya mbu,inatajwa iwapo ingetumika miezi kadhaa iliyopita ingesaidia kupunguza idadi ya waliougua ugonjwa wa dengue.

Hayo yalibainishwa na Meneja Ubora wa TBPL Samuel Mziray,  alipokuwa akingumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, wakati wa maonyesho ya nne ya bidhaa katika wiki ya viwanda vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC)yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Tatizo la kisera nchini ilikuwa na afua yake ambayo ni vyandarua kuwekewa viatilifu,ndiyo lililokwamisha dawa hiyo isinyunyizwe,” Mziray alisema.

Alibainisha kuwa pamoja na hayo wamepata taarifa kuwa Wizara ya Afya imejipanga kuanzia mwaka huu wa fedha kutenga bajeti itakayowezesha dawa hiyo kusambazwa nchini.

Alibainisha viuadudu wanayotengeneza vina ubora kwa kiwango cha asilimia 100, na kuwa  imethibitishwa na mamlaka husika ambapo ilisimamiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Alisema nchi tatu miongoni mwa wanajumuiya wa SADC za Angola, Eswatini,na Msumbiji zimeonyesha nia ya kuingia mkataba na kiwanda hicho ili kununua dawa hizo katika hatua ya kudhibiti mbu na ugonjwa wa malaria kwenye nchi zao.

Afisa Masoko wa TBPL, Michael Nyangasa, alisema kiwanda hicho pekee barani Afrika cha TBPL, kilianza uzalishaji wa viuadudu Desemba mwaka 2017 ikiwa ni zao la teknolojia kutoka Cuba.

Alisema  dawa hiyo ni nafuu, hivyo ikitumika vyema na jamii, itasaidia kuwapunguzia hatari ya kuugua malaria pamoja na kuepuka gharama za matibabu.

Alisema pamoja na kuhamasisha usafi wa mazingira, pia huwashauri wananchi kutumia dawa hiyo kwa kuweka matone 20 katika kila lita 50 za maji yaliyopo kwenye matenki, makaro na vyombo vya kuhifadhia maji kwa kuwa ni sehemu za mazalia ya mbu.

Alisema pia bado maji hayo yatakuwa salama kwa matumizi yao.

Habari Kubwa