Tanzania ina haki ya kuvuna mema SADC

13Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tanzania ina haki ya kuvuna mema SADC

MKUTANO wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)unafanyika nchini  ambapo tunatarajia viongozi wakuu 16 wa nchi na serikali za nchi hizo wanachama watahudhuria.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo yenye historia ya aina yake. Ni miongoni mwa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi na mapambano dhidi ya ubaguzi na utawala dhalimu uliokuwa katika nchi kadhaa za kusini mwa Afrika.

Chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Tanzania iliongoza mapambano kusini mwa Afrika, baadhi ya viongozi kadhaa wa nchi zilizotawaliwa kwa mabavu walifika na kupewa mafunzo au hifadhi ya muda ili kujipanga vyema kwa mapambano.

Mara kadhaa baadhi ya viongozi wa nchi hizo ikiwamo Msumbiji hawakusita kubainisha jinsi ambavyo walijisikia huru wakiwa kwenye hifadhi zao kwa kuwa hata wananchi wa kawaida waliwapa ushirikiano mzuri.

Baada ya ukombozi wa nchi zilizokuwa katika ukoloni pamoja na ubaguzi wa rangi hususan Afrika Kusini, sasa  SADC imekusudia kujitafutia maendeleo na ustawi wa jamii miongoni mwa nchi wanachama, ikiwa ni mtangamano wa kikanda.

Mtangamano huo una hatua tano, ambazo zinatajwa kuwa ni soko la pamoja, umoja wa forodha, umoja wa kiuchumi, eneo huru la biashara na shirikisho la kisiasa.

Nchi za Sadc zimejiwekea malengo ambayo ni n kufikia eneo huru la biashara ifikapo mwaka 2008, umoja wa forodha (2010), soko la pamoja (2015), umoja wa fedha (2016) na hatimaye kuwa na sarafu moja mwaka 2018.

Mkutano wa wakuu wa serikakli na nchi umetanguliwa na maonyesho ya Nne ya viwanda SADC ambapo wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji walipata fursa ya kushiriki.

Maonesho hayo yamefuatiwa na mijadala mbalimbali ya kimaendeleo katika nyanja tofauti, ikiwamo uwezeshaji wa viwanda, kukuza soko la bidhaa na ubora wa bidhaa husika, huduma za maendeleo ya jamii, siasa na usalama.

Kutokana na mazingira yalivyokuwa kwenye maonesho hayo, ni wazi kwamba wananchi wengi hawakupata fursa ya kushiriki, lakini wale wachache walioshiriki wanaweza kufikisha jumbe mzuri kwa wenzao.

Kwa upande wa taasisi, tumejulishwa kuwa Bohari Kuu ya Dawa imepata jukumu la kununua dawa na kuzipeleka kwa nchi wanachama kulingana na makubaliano waliojiwekea.

Kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluilui vya mbu nchini cha Tanzania Biotech Product (TBPL) tayari kimeanza kung’ara kwa nchi za SADC baada ya nchi hizo kutangaza nia ya kununua viuadudu hivyo.

Kuanzia leo tumaamini kuwa mambo mengi na makubwa yatafanyika kutokana na kuanza kwa vikao kadhaa kuanzia vya makatibu wakuu, mawaziri hadi kilele chake ambacho viongozi wakuu watakutana.

Miongoni mwa mambo yatakayofanyika ni kubadilishana nafasi za uongozi wa jumuiya, huku Rais John Magufuli akitarajiwa kukabidhiwa uenyekiri ataodumu nao kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Rais Hage Geingob wa Namibia anayemaliza muda wake ndiye atakabidhi kijiti kwa Rais Magufuli ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa SADC.

Tunaamini kwamba Rais Magufuli ataiwakilisha vyema Tanzania, na ni matarajio yetu kwamba chini ya uongozi wake makini,  kwa nafasi hiyo, SADC itapiga hatua kadhaa kutoka hapo ilipo na kusogea mbele.

Ni matarajio yetu kuwa baada ya mkutano huu, SADC itapaa kwa kasi ili kufikia malengo ambayo wanachama wamejiwekea.

Habari Kubwa