Ajali ya Morogoro iturudishe kwenye maadili si vinginevyo

13Aug 2019
Raphael Kibiriti
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ajali ya Morogoro iturudishe kwenye maadili si vinginevyo

NIANZE kwa kuungana na wananchi wenzetu wa mkoa wa Morogoro na wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na msiba mzito uliolikumba taifa letu, kufuatia vifo vya Watanzania 71 kwa takwimu za hadi jana asubuhi.

NIANZE kwa kuungana na wananchi wenzetu wa mkoa wa Morogoro na wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na msiba mzito uliolikumba taifa letu, kufuatia vifo vya Watanzania 71 kwa takwimu za hadi jana asubuhi.

Ni vifo vilivyotokana na ajali ya moto ya Agosti 10, baada ya gari lililokuwa limebeba petroli kupinduka eneo la Msamvu ambapo baadhi ya watu walilivamia na kufungua koki zake ili waibe mafuta hayo.

Katika mchakato huo usio halali, moto ulilipuka na kuwaunguza wote waliokuwa katika ‘fursa’ ya kuiba mafuta hayo.

Ni bahati mbaya kwamba, baadhi ya watu waliokuwa katika shughuli zao halali za kila siku nao wameathirika.

Muungwana anaungana na hatua zilizochukuliwa na serikali za kuwahudumia waliothirika na ajali hiyo, wakiwamo waliopoteza maisha.

Mbali na kuendesha operesheni ya kitaifa ya kuwahifadhi waliofariki, lakini kupitia kwa Rais John Magufuli, serikali imebeba gharama zote za kuwatibu majeruhi, huku ikitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.

Ni mengi yamezungumzwa kwa namna tofauti kuhusiana na kadhia hiyo kwa mtazamo chanya lakini pia mtazamo hasi.

Wapo wanaovinyooshea vidole vyombo vya ulinzi na usalama vyenye dhamana ya kuhakikisha kuna ulinzi na usalama wa maisha na mali za watu katika mazingira yote, yakiwamo yale yanayohusisha ajali mbalimbali kama hii iliyotokea.

Wanavinyooshea vidole kwamba havikutimiza wajibu wao na ndiyo maana kadhia hiyo ikatokea.

Wakati Muungwana akiungana na Rais Magufuli kwamba huu si wakati wa kunyoosheana vidole kulaumiana, bali kutoa kipaumbele kwa matibabu ya majeruhi, anadhani kuna somo kwa Watanzania la kuendelea kujifunza.

Kuendelea kujifunza kuwa ‘utamaduni’ usio wa kimaadili tunaozidi kuuendekeza kwa kasi ya ajabu wa kuvamia magari yanayopata ajali ili kuiba na si kutoa msaada, utazidi kutuangamiza tusipobadilika.

Imeripotiwa mara nyingi kwenye vyombo vya habari jinsi watu wanavyovamia na kupora mali za majeruhi wa ajali.

Na mbaya zaidi badala ya kutoa msaada, wengine wanadaiwa hata kufikia hatua ya ‘kuwamalizia’ kabisa majeruhi ili tu waweze kuwaibia mali walizonazo.

Muungwana ambaye anaishi eneo la Wazo Hill jijini Dar es Salaam ameshuhudia mara nyingi, jinsi magari yaliyofeli breki yanavyokimbiliwa na watu.

Yanakimbiliwa si kwa ajili ya kwenda kutoa msaada katika mtelemko wa barabara ya Wazo kwa wanaoifahamu, ila kwenda kuiba mifuko ya simenti, gari itakapoanguka.

Si upande wa magari ya simenti tu, kuna matukio kwa mfano katika barabara ya Nelson Mandela inayopitisha magari yanayobeba mafuta kutoka ama kwenda kuchukua mafuta bandarini.

Kuna watu ambao hufungua koki ya magari hayo ili kukinga mafuta wakati mwingine wakitumia mifuko ya nailoni, katikati ya misururu ya magari.

Aidha, imeshuhudiwa namna ambavyo watu huvamia gari zilizopata ajali zikiwa na vinywaji kama bia na kuiba kreti za vinywaji, wengine ‘wakipoza’ makoo yao bila ya kujali kwamba huo ni wizi.

Mbali na bidhaa kama za petroli,  barabara hizi husafirisha pia bidhaa kama kemikali za sumu na milipuko ambayo yote ni ya hatari.

Muungwana anasema ni somo la kuendelea kutoa funzo kwamba kuita ajali kama hizi kuwa ni ‘fursa’ ya kujineemesha kwa namna yoyote ile ni kinyume cha maadili ya kiasili ambayo kila binadamu ameumbwa nayo.

Maadili ya kujua chema na kibaya, kwamba haihitajiki kwa kweli hadi aje polisi ama ofisa yeyote wa serikali kumwambia mtu kuwa kitendo cha kuchukua dumu nyumbani kwake kwenda kuiba mafuta ya gari lililopata ajali hakikubaliki.

Wakati waathirika wa ajali hiyo wanaendelea kutibiwa, Muungwana anaasa Watanzania kurudi kwenye maadili na utamaduni wa kusaidia watu wanaopatwa na ajali, badala ya kuchukulia ajali kama fursa.

Anasema, siri ya mafanikio ni kufanya kazi halali, si vinginevyo.

Habari Kubwa