Wahimizwa kusaidia makundi yasiyojiweza

13Aug 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Wahimizwa kusaidia makundi yasiyojiweza

WATANZANIA wametakiwa kujenga tabia ya kusaidia makundi yasiyojiweza hususani watoto yatima wanaokabiliwa na changamoto za kimaisha, ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea kama watu wengine.

Wito huo ulitolewa jana na Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wa Jiji la Arusha, Sarah Mwangasa, wakati alipokuwa katika hafla fupi ya ugawaji wa msaada wa sare za shule, mabegi na vyakula uliotolewa na kikundi cha kijamii cha Friends of Batuli, kwa wanafunzi yatima wanaosoma katika shule za msingi Osunyai na Sombetini katika Halmashauri na Jiji la Arusha.

Mwangasa alisema wapo watoto wengi wasiojiweza wanaosoma katika shule 48 za Jiji la Arusha ambao wanakabiliwa na changamoto za kukosa mahitaji muhimu ya kimaisha ili wafanikiwe kufikia malengo ya kielimu.

"Natoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa kujitolea kusaidia jamii kadiri wanavyobarikiwa na Mwenyezi Mungu ili watoto hawa wafanikiwe kufikia malengo yao," alisema.

Awali, msemaji wa kundi la Friends of Batuli, Mwalimu Batuli Kisaya, alisema kundi hilo limeanzishwa mahususi kwa lengo la kusaidia jamii hususani watoto yatima na wenye mahitaji maalumu, kupitia michango yao.

Alisema kuwa kundi hilo limeguswa na watoto yatima wanaosoma katika shule hizo, baada ya kubaini kuwa wanakabiliwa na changamoto ya uhitaji wa vitendea kazi vya shuleni na kuamua kuhamasishana kuwachangia watoto hao.

"Kundi letu limejikita kuhamasisha jamii kwa vitendo ili kusaidia makundi maalumu, kwa ajili ya kuwawezesha na wao waweze kupata faraja na kuishi kama watoto wengine wanaolelewa na wazazi wao," alisema Batuli.

Alisema kikundi hicho, kiligawa msaada wa mabegi ya shule, sare za shule na vyakula kwa wanafunzi wapatao 59 na msaada huo umegharimu Sh. milioni 1.5.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi waliopatiwa msaada huo, Robert Jacob na Jeremiah Daniel, kutoka shule za msingi Osunyai na Sombetini, walishukuru kwa msaada huo na kuomba Watanzania kuwakumbuka makundi maalumu yenye mahitaji kama wao.

Habari Kubwa