Wakulima, wafugaji Kanda ya Kaskazini kupima kisasa

13Aug 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Wakulima, wafugaji Kanda ya Kaskazini kupima kisasa

WAKULIMA na wafugaji wa Kanda ya Kaskazini wametakiwa kulima kilimo cha kisasa ili wapate mavuno mengi yenye tija kwao na taifa, ili kupata malighafi kwaajili ya viwanda na kukuza uchumi.

wakulima na wafugaji

Akizungumza jana kwenye maonyesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyomalizika kwenye viwanja vya Themi jijini hapa Agosti 12, mwaka huu, Mratibu wa mauzo wa kampuni ya mbegu ya Kibo Seed, Hassan Kimweri, alisema anawaomba wakulima na wafugaji kulima kwa kutumia kanuni bora za kilimo cha kisasa ili wavune mavuno mengi na bora.

Alisema endapo wakulima na wafugaji watapata mazao bora wataweza kuuza nje ya nchi baada ya kuandika na kupata fedha za kigeni.

"Maendeleo ya viwanda yanayotamkwa kila siku na serikali ya awamu ya tano yanategemea sana malighafi bora na za kutosha kutoka kwa wakulima na wafugaji, sasa tusipolima na kufuga kwa kutumia mbinu bora na za kisasa za kilimo itakuwa ndoto, tutafaulu tukilima kisasa na kusikiliza wataalamu wa kilimo na kutumia mbegu bora," alisema Kimweri.

Alisema viwanda vinavyoendelea kujengwa vinahitaji kwa wingi malighafi kama za kusindika sharubati (juisi), nyanya za kopo, matikiti maji, mahindi kwaajili ya unga na vyakula vya mifugo, nyama bora za ng'ombe na mbuzi pamoja na mbogamboga.

Kimweri alisema wakulima hawana budi kuamka usingizini na kuziendea benki zinatoa mikopo ya kilimo na ufugaji ili kupata pembejeo bora ikiwamo mbegu bora.

Alisema wakulima na wafugaji ni kivutio cha watalii kwa kuwa wanapotembelea hoteli za kitalii wanategemea mazao bora ya wakulima kutoka mashambani kwaajili ya mlo zikiwamo mboga, matunda na nyama.

"Wakulima wanatakiwa kwakweli kubadilika na kuwa na mtazamo chanya kwa kuacha kilimo cha kizamani, wanategemewa na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, maana asilimia 71 ya Watanzania ajira zao zipo kwenye kilimo na ufugaji, sasa tusipobadilika tutachezea uchumi wetu tu," alisema Kimweri.

Alisema Kampuni ya Kibo Seed Co. imeshinda nafasi ya kwanza kwa kampuni ya mbegu ya Kanda ya Kaskazini, kwenye maonyesho ya Nanenane ya mwaka 2019 kutokana na mbegu bora wanazotoa ambazo zimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima kwa kuwapatia mavuno mengi na bora.

Pia, wamekuwa na wataalamu wanaotembelea wakulima wanapokuwa wameanza msimu wa kilimo na kuwafundisha kanuni bora za kilimo.

Kimweri alisema kampuni yake katika maonyesho ya Nanenane mwaka huu, imealika vikundi vya wakulima kutoka Mwanza, Singida na Tanga kuja kujifunza na kupata uzoefu wa wakulima na kampuni zingine za mbegu.

Alitaja mbegu zinazotumiwa na wakulima sehemu mbalimbali  nchini, kuwa ni za mahindi, vitunguu, nyanya, mbegu za majani ya ng'ombe na mbogamboga.

Habari Kubwa